SUAMEDIA

Naibu Waziri Masauni awataka Vijana kuchangamkia Fursa za Uchumi wa Blue Zanzibar

 Na Benny Mwaipaja, Zanzibar

NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amewahimiza vijana Visiwani Zanzibar kuchangamkia fursa za uchumi wa blue unaotokana na shughuli za uvuvi na uchakataji wa samaki ili waweze kujikwamua kiuchumi.



Mhe. Masauni ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni-Zanzibar, ametoa rai hiyo wakati akizungumza na viongozi na baadhi ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi katika Jimbo la Kikwajuni akiwa katika ziara yake ya kikazi visiwani humo.

Amesema kuwa yeye binafsi na Mwakilishi wa Jimbo hilo katika Baraza la Wawakilishi Mhe. Nasor Ali Jazeerah pamoja na viongozi wengine wamejipanga kutoa vifaa vitakavyotumiwa na vijana kwa ajuili ya shughuli za uvuvi katika sekta hiyo ya uchumi wa blue ili waweze kujitegemea kwa kujipatia kipato cha uhakika.

“Tunataka tuangalie uwezekano wa kujenga mazingira mazuri ya kuwatafutia “ndoano” na siyo “samaki” na tumeandaa vitu vikubwa ambavyo sitaki niseme mapema hapa nitaondoa radha, mkawaambie vijana wa Kikwajuni kama hawatatoka kimaisha kipindi hiki hawatatoka maisha” alilisisitiza Mhe. Masauni.

Pamoja na kusisitiza masuala ya kiuchumi, Mhandisi Masauni alisema kuwa mipango mingine iliyowekwa na uongozi katika Jimbo la Kikwajuni ni kuendesha mashindano ya kusoma qoran kwa vijana na kuwataka wazazi kuwahimiza watoto wao kushiriki mashindano hayo.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo hilo Mhe. Nasor Ali Jazeerah, aliwaahidi wakazi wa Jimbo la Kikwajuni-Zanzibar kwamba ahadi zote zilizoahidiwa wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita zitatekelezwa kikamilifu.

Alitoa wito kwa wakazi wa Jimbo hilo kushikamana, kupendana na kuacha majungu ili mipango ya maendeleo iliyopangwa iweze kutekelezwa kwa kasi zaidi.

Aliwashukuru wananchi kwa kumwombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ili waendelee kuingoza nchi kwa umahili mkubwa.

Post a Comment

0 Comments