SUAMEDIA

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro aagiza wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kutengeneza nyaraka feki na kuuza ardhi kinyemela Mvomero

 


Na: Vedasto George

Wananchi wa kijiji cha Vianzi kata ya Lubungo wilayani Mvomero Mkoani Morogoro wameulalamikia Uongozi wa kijiji hicho wakiutuhumu kwa kutengeneza nyaraka feki na  kuuza ardhi kinyemela pasipo kuwashirikisha na kusababisha migogoro isiyo ya lazima.

Wakizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa huo Loata Ole Sanare wakazi wa kijiji hicho wamesema wameshindwa kufanya shughuli za kilimo pamoja na miradi ya maendeleo wakihofia kuchukuliwa mashamba yao na uongozi wa kijiji ambao umekuwa ukighushi nyaraka na kuuza mashamba ya kijiji pasipo kufuata utaratibu.

“Kijiji ni cha kwetu lakini sisi hatuna mashamba wamepewa wawekezaji na tunakodishiwa hayo mashamba kwa sh. 40,000/=, hii ndio kero yetu sisi wanakijiji wa Vianzi, kwa kweli tumeyumba kiuchumi hatuna fedha za kukodisha mashamba kwa hiyo hata ikifika kipindi cha mavuno inatugharimu tena kununua mahindi wakati tungeweza kulima wenyewe,  sasa hivi mahindi yamepanda bei debe moja tunanunua sh.15,000/=”, alisema mmoja wa wanakijiji Bw.Kasubi Sospeter.

Kwa upande wake Msimamizi Mkuu wa Lanchi ya Dakawa na Mkata Oscar Mengele amesema baada ya kufanya ufuatiliaji wamebaini kuwepo kwa baadhi ya wawekezaji ambao tayari wameuziwa eneo lenye ukubwa wa hekta 700 za lanchi hiyo.



“Kuna baadhi ya maeneo ambayo kimsingi yamevamiwa kwa maana wamepewa wawekezaji bila kufuata utaratibu, unakuta mtu ana hekta karibia 2,000, au hekta 500 na kuendelea lakini hawa wote hawakufuata utaratibu, eneo lililovamiwa mpaka sasa ni hekta 7,000”,alisema Msimamizi huyo.


Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare akiwa ameambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama wamesema wahusika wote watachukuliwa hatua za kisheria huku Mkuu wa wilaya ya Mvomero Albinus Mgonya akisema migogoro hiyo isiyo na tija haitokuwa na nafasi katika wilaya hiyo.

“Wapo watu ambao walitoa hatimiliki za kimila  na hawajawahi kufika Vianzi hawajui kitu kinachoitwa Vianzi lakini wametoa hatimiliki, kuna bwana mmoja anaitwa  Majaliwa  Jafari yupo halmashauri hapo Mvomero, Jafari kwenye hati nilizo zikamata hakuna mihutasari ya kijiji wala ya wananchi, lakini ametoa hati za kimila zisizopungua 21 mpaka leo ambazo wananchi hawajajadili”,alisema Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.


       







Post a Comment

0 Comments