SUAMEDIA

Magazeti yatoa mchango mdogo katika kutoa Taarifa za Tabianchi

 Na: Calvin E. gwabara

Imebainishwa kuwa  mchango wa Magazeti kwenye kutoa habari na taarifa mbalimbali zinazohusu masuala ya mabadiliko ya tabia nchi  Tanzania ni kidogo kutokana na taarifa kidogo  zinazoandikwa na magazeti hayo kila siku ikilinganishwa na masuala mengine kama siasa na burudani.





Hayo yamebainishwa kupitia utafiti wa Mwanafunzi wa kwanza kujisajili kusoma Shahada ya Uzamivu kwenye Idara ya taarifa na kumbukumbu  katika Maktaba ya Taifa ya Kilimo (SNAL) Bwana Peter Onauphoo Siyao wakati akitetea utafiti wake uliomuwezesha kupata shahada ya Udaktari wa falsafa.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti wake mbele ya jopo la walimu  watano, Dkt. Siayo ambaye ni mfanyakazi kwenye Maktaba ya Chuo Kikuu cha Mzumbe alikuwa anafanya utafiti kuangalia mchango wa vyombo vya habari kwa maana ya magazeti katika kutoa taarifa na elimu kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabia nchi nchini Tanzania.

Kwenye utafiti wake  amebaini kuwa pamoja na magazeti kuwa na uwezo mkubwa katika kusaidia kutoa taarifa na elimu ya kina kwa jamii kuhusu masula ya mabadiliko ya tabia  nchi lakini vyombo hivyo vya habari nchini havitoi nafasi ya kuchapisha habari na makala mbalimbali zinazohusu masuala hayo hapa nchini ipasavyo.

Katika utafiti wake amefanikiwa kuchapisha machapisho manne kwenye majarida ya kimataifa ambapo chapisho la kwanza liliangalia namna vyombo hivyo vya habari vinavyotoa nafasi kwenye habari za mabadiliko ya tabia nchi na kubaini kuwa magazeti yanatoa habari kidogo ukilinganisha na habari za masuala mengine.

Chapisho lake la pili aliangalia umuhimu unaopewa na habari za mabadiliko ya tabia nchi na kubaini kuwa habari hizo hazipewi umuhimu kwenye magazeti ya Tanzania na hivyo kuchangia kidogo kwenye kutoa elimu na taarifa ya masuala hayo kwa jamii.

Mwanafunzi huyo kwenye Chapisho lake la tatu  kwenye utafiti wake aliangalia vyanzo vya taarifa vya magazeti hayo katika kupata taarifa zinazohusu masuala ya mabadiliko ya tabia nchi na kubaini kuwa ni asilimia  64.0% ya wataalamu wa masuala ya mabadiliko ya tabia nchi walihusihwa na asilimia 34.1% ya matukio ya kila siku ya masuala hayo ndio yaliwawezesha kupata habari hizo huku wakikumbana na changamoto nyingi kwenye kupata taarifa hizo.

Katika chapisho lake la nne aliangalia matumizi ya magazeti kwa watu waishio vijijini katika kupata taarifa za mabadiliko ya tabia nchi na kugundua kuwa magazeti yanatumiwa kwa asilimia 65% na watu wa vijijini kwenye kupata taarifa hizo.

Katika utafitii huo bwana Siayo amefanikiwa kupata Shahada yake ya Uzamivu  na sasa kuwa Daktari rasmi baada ya jopo lote kuridhika na utafiti wake aliouwasilisha na kuthibitisha kuwa  mchango wa Magazeti kwenye kutoa habari na taarifa mbalimbali zinazohusu masuala ya mabadiliko ya tabia nchi  Tanzania ni kidogo kutokana na taarifa kidogo zinazoandikwa na magazeti hiyo kila siku ikilinganishwa na masuala mengine kama siasa na burudani.

 

 

Post a Comment

1 Comments

  1. Mwandishi Msomi wa Sua anaandika sentensi ndefu sana. Yaani paragraph moja ni sentensi moja.

    ReplyDelete