SUAMEDIA

Mafunzo kwa Waelimishaji Rika SUA chachu ya kupunguza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na Magonjwa Sugu yasiyoambukiza

 NA CALVIN GWABARA

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA waliopata nafasi ya kupata mafunzo ya uelimishaji rika chuoni hapo wametakiwa kuhakikisha wanayatumia mafunzo hayo vyema kwa kutoa elimu kwa wenzao ili kusaidia kupunguza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na Magonjwa Sugu yasiyoambukiza.

Daktari Kiongozi wa Hospitali za SUA na Mkuu wa Idara za Huduma za Hospitali Dkt. Omari Kasuwi akifungua mafunzo ya Waelimishaji Rika chuoni hapo.


Wito huo umetolewa Dkt. Omar Kasuwi ambaye ni Daktari Kiongozi wa Hospitali za SUA wakati akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika Chuoni hapo na kuwakutanisha wawakilishi wa wanafunzi kutoka kozi mbalimbali kutoka kampasi zote za SUA mkoani Morogoro.

“Elimu hii mnayoipata ninyi leo ya uelimishaji rika lengo lake kubwa ni kuwawezesha kuwa mabalozi kuhusu masuala ya ukimwi na magonjwa mengine sugu kwenye maeneo yote mnayotoka iwe kwenye kozi zenu, mabweni yenu na hata kwenye kampasi mnazotoka ndio maana mafunzo hayo yamezingatia mchanganyiko mzuri ambao unagusa kila kona, hivyo hakikisheni elimu hii mnaifikisha kwa wenzenu ili kwa pamoja tuchangie kuongeza uelewa kuhusu magonjwa haya”, alisisitiza Dkt. Kasuwi.

Dkt. Kasuwi amesema kuwa pamoja na dhamira na uwekezaji mkubwa ambao unafanywa na familia na serikali katika kuwapatia vijana elimu na ujuzi ili hatimaye waweze kusaidia familia na taifa kwa kucnagia kwenye maendeleo lakini ndoto hizo kwa wengine hufutika kutokana na athari za maambukizi ya VVU/UKIMWI na Magonjwa sugu yasiyoambukiza (MSY).

Aidha ameongeza kuwa pamoja na hilo lakini kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2016/2017 umeonesha kuwa sehemu kubwa ya maambukizi mapya ya VVU yanatokea kwa vijana wenye umri kati ya miaka 15-23 kundi ambalo wengi wao wapo vyuoni  na kwamba utafiti pia ulibaini wanafuinzi wa vyuo vikuu wako katika hatari zaidi ya kupata maambukizi.

Dkt. Kasuwi ameendelea kusema kuwa mwaka 2013 serikali ilifanya tathimini ili kubaini iwapo mikakati ya kudhibiti UKIMWI iliyokuwepo imeleta mafanikio yaliyokusudiwa hasa kwa watumishi wa Umma na matokeo hayo ya utafiti yalibainisha kuwa UKIMWI na MSY ulichangia sana kwenye vifo hivyo na kuathiri utendaji katika utumishi wa Umma.

Amesema utafiti huo ulipelekea  serikali kutoa waraka namba 2 wa mwaka 2014 uliowataka waajiri wote kuweka mikakati na kusimamia mikakati ya udhibiti wa UKIMWI na MSY sehemu za kazi ili kupunguza athari zake.

Dkt. Kasuwi amebainisha kuwa tangu kuanza mapambano dhidi ya magonjwa hayo Chuo cha SUA kimeendelea kuwa kinara katika mipango na mikakati ya utekelezaji wa waraka na maagizo hayo ya serikali miongoni mwa vyuo vikuu vyote nchini na ameahidi kuendelea na jitihada hizo ili kuhakikisha wanafunzi na wafanyakazi wote wanakuwa salama wakati wote ili kutimiza ndoto zao na kutimiza malengo ya kila mfanyakazi ili kuleta maendeleo.

Awali akizungumza kuhusu mafunzo hayo kwa waelimishaji rika chuoni hapo Mratibu wa UKIMWI na Magonjwa sugu yasiyoambukiza SUA Dkt. Erhard Kapilima amesema sababu kuu za mafunzo hayo ni kutekeleza maelekezo ya waraka huo na kwamba  miaka michache iliyopita magonjwa hayo yameongezeka kwa kasi na hiyo imetokana na kulegalega kwa mkazo kwenye kutoa elimu na kusimamia magonjwa hayo hivyo kufundisha waelimishaji rika kutasaidia kuongeza uelewa kwa jamii ya wanafunzi.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yameanza kwa jamii ya wanafunzi chuoni hapo lakini zoezi lingine kama hilo litafanyika pia kwa watumishi wa SUA watakaochaguliwa kulingana na maeneo yao ya kazi ili pia wapewe mafunzo na kupata waelimishaji rika hao kila kona ya chuo ili kuwe na nguvu ya pamoja ya kutoa elimu na kupunguza maambukizi ya magonjwa hayo.

Dkt. Kapilima amesema mafunzo hayo kwa wanafunzi yamekuwa yakitolewa kila mwaka kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wa pili ili kusaidia kuziba pengo la wale wanaomaliza mwaka wa tatu na kukifanya chuo kuendelea kuwa na waelimishaji rika wa kutoka kila mwaka chuoni hapo na kusaidia mapambano ya kuyakabili magonjwa hayo.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa SUA Heath Club Bw. Musa Katyeka amesema mafunzo hayo yamekuwa muhimu sana kwao kama wanafunzi kwani yamewasaidia kuwapatia wataalamu wengi wa kujitolea kutoa elimu kwa wanafunzi wenzao chuoni hapo juu ya magonjwa hayo na hivyo kuchangia kupunguza maambukizi miongoni mwao.

Kyateka ameongeza kuwa wao kama wanafunzi kila mwaka wanapata wanafunzi wengine wapya chuoni wengine wakiwa na umri mdogo hivyo ni muhimu kuwa na mafunzo ya aina hiyo ili kusaidia kupata idadi ya kutosha kuhudumia idadi kubwa ya wanafunzi wenzao kwenye mambo ya msingi ya namna ya kujikinga na maambukizi ili waweze kufikia ndoto zao na kuchangia kwenye maendeleo ya taifa.

Katika mafunzo hayo ya siku moja yaliyoandaliwa na SUA kupitia Idara ya Huduma za Hospitali,  washiriki watajifunza mada  mbalimbali kutoka kwa madaktari bingwa wa magonjwa hayo pamoja na kupata shuhuda za watu wanaoishi na VVU mkoani Morogoro ambao nao watapata nafasi ya kuzungumza na wanafunzi hao.

  Mratibu wa UKIMWI na Magonjwa Sugu yasiyoambukiza SUA Dkt. Erhard Kapilima akitoa maelezo ya maengo ya mafunzo hayo kabla ya ufunguzi rasmi wa mafunzo kwa Waelimishaji Rika SUA.

  Daktari Bigwa wa Wanawake  na Uzazi ambye pia ni Daktari Kiongozi wa Hospitali ya SUA upande wa Mazimbu Dkt. Elimwidimi Swai akitoa mada yake kuhusu UKIMWI na Virusi vya Ukimwi VVU.

 

 Washiriki wa mafunzo SUA  ya uelimishaji rika wakichangia na kufuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa kwenye mafunzo hayo ya siku moja chuni hapo.

 

                                           

3.     

4.     

 

 

 

Post a Comment

0 Comments