Gerald Lwomile
Tukuyu
Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesema inaona kuna fursa
kubwa ya kuwajengea uwezo wafugaji katika maeneo mbalimbali ili kujua
uendelezaji wa malisho bora ambayo yatamuhakikishia mfugaji kuwa na afya bora
lakini pia kuongeza kipato cha kaya
Hayo yamesemwa wilayani Rungwe mkoani Mbeya na Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo, na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angelo Mwilawa wakati akizungumza na SUA Media mara baada ya Warsha ya siku moja iliyoandaliwa na mradi wa Innove Afrika unaolenga katika kuhakikisha kunakuwa na uhakika wa chakula
Dkt. Mwilawa amesema kuwa hatua hiyo ya kuwaendeleza
wakulima imekuwa ni muendelezo wa maagizo
kutoka kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Mashimba Ndaki ambaye amekuwa akitaka
kuhakikisha Wizara anayoongoza inatoa elimu ya kutosha kwa wakulima
Akizungumzia malisho ya nyasi aina ya Brachiaria
ambazo zimefanyiwa utafiti na watafiti kutoka Mradi wa Innove Afrika ulio chini
ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Dkt. Mwilawa amesema ni Mradi wenye
mafanikio makubwa na kuwataka wafugaji katika wilaya hiyo na kote nchini
kuhakikisha wanaendeleza teknolojia hiyo kwa kupanda na kustawisha nyasi hizo
“Na hili ambalo tumeliona, aina hii ya malisho ya Brachiaria ni moja ya aina ya nyasi za malisho ambazo zimefanyiwa utafiti nchini lakini kwa sasa tumeona aina hii ya malisho ina ubora mkubwa katika kuleta lishe bora kwa mifugo”, amesema Dkt. Mwilawa
Naye mmoja wa watafiti katika Mradi huyo Dkt. Ismail
Suleiman amesema kuwa teknolojia hiyo imepokewa vizuri na wafugaji wengi
wilayani Rungwe mkoani Mbeya kwani kwa sasa wafugaji wameamka na kuanza kupanda
malisho hayo
Amesema mradi ulianza na wafugaji wachache lakini kwa
sasa idadi imekuwa ikiongezeka siku hadi siku kiasi kwamba wapo wafugaji
waliamua kupanda malisho hayo wakati wa kiangazi na kumwagilia kwa maji ili
kuhakikisha wanakuwa na malisho hayo
Mmoja wa wanufaika ambaye aliamua kupanda wakati wa
kiangazi Bw. Anyabwile Asa Mwakosya amesema awali alikuwa akichukua nyasi
porini na kwa kiasi kikubwa zilileta madhara kwa mifugo yake
“Awali nilikuwa nikikata majani porini na wakati mwingine ng’ombe alipokula mimba ilikuwa na uwezo wa kutoka na hata sikujua kwa nini, lakini kwa sasa tangu nianze kutumia nyasi hizo wanyama wangu mimba huenda kwa wakati muafaka pasipo kuvurugwa”, amesema Mwakosya
Mradi wa Innove Afrika unajumuisha nchi sita barani Afrika zikiwemo nchi za Tanzania na Kenya.
0 Comments