SUAMEDIA

Naibu Waziri Waitara awaagiza wenye Viwanda nchini kuajiri Wataalamu Wa Mazingira

 Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mwita Waitara amewaagiza wenye viwanda wote nchini kuajiri wataalamu wa mazingira ili kukidhi matakwa ya kisheria.



Waitara ametoa maagizo hayo alipofanya ziara ya kikazi ya kutembelea viwanda mbalimbali vilivyopo maeneo ya Mlandizi na Kibaha wilayani Kibaha mkoani Pwani kwa lengo la kukagua uzingatia wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004.


Aidha ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufanya ukaguzi wa mazingira katika viwanda vilivyopo wilayani humo ili kuona kama wanatunza mazingira kisha kuandaa ripoti itakayoisaidia Serikali kutoa maamuzi ili kuwalinda wananchi na uchafuzi wa mazingira.

Pamoja na kuwapongeza wawekezaji wa viwanda aliwataka kufuata sheria na kusisitiza kuwa Serikali haitafungia kiwanda chochote na badala yake itawasaidia kukidhi matakwa ya sheria.

Hata hivyo kutokana na hali aliyoikuta alipotembelea na kukagua kiwanda cha Keds Tanzania Company Ltd alikutana na utiririshaji wa majitaka bila kuyatibu jambo linaloweza kusababisha athari kwa mazingira na wananchi ambapo alisema ni kosa kisheria.

Kutokanana hali hiyo Waitara alitoa siku 14 kwa kiwanda hicho kuyafanyia kazi maagizo waliyopewa na NEMC na kuhakikisha wanaacha mara moja kutiririsha maji hao sambamba na kuwa na mtambo wa kuchakata taka ambazo wanazalisha ili kuepusha kusambaa hovyo kwa taka.

Post a Comment

0 Comments