SUAMEDIA

 

Na Gerald Lwomile

Morogoro

Serikali ya mkoa wa Morogoro imesema haitawavumilia watendaji wake wakiwemo watumishi wa Halmashauri zilizoko mkoani humo ambao hawatachukua hatua za makusudi katika kuhakikisha vijana wanazitumi fursa zilizopo katika kujiletea maendeleo


Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe. Ismail Mlawa waliokaa (katikati) na Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Injinia Emmanuel Kalobelo wa pili kutoka kulia wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki mbalimbali katika uzinduzi wa mradi wa "Uchumi" wengi kulia ni Mwakilishi wa Mkurugenzi wa SAGCOT John Mbaga na aliyekaa wa pili kushoto ni Msimamizi wa Miradi wa CARE INTERNATIONAL Bi. Haika Mtui

Agizo hilo limetolewa Machi 12, 2021 na Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Injinia Emmanuel Kalobelo wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa Mradi wa Vijana ni Uchumi Imara, mradi uliozinduliwa mkoani Morogoro

Injinia Kalobelo amesema kuwa mkoa wa Morogoro umekuwa na fursa nyingi ikiwemo ardhi, viwanda zaidi ya 3,370 ambapo amesema hiyo ni fursa kubwa kwa vijana katika kuhakikisha wanainua uchumi wao na familia kwa ujumla.

Naye Mgeni Rasmi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe. Ismail Mlawa ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro amesema kuwa lengo la mradi huo ni zuri kwani litasaidia kuunganisha vikundi vya kiuchumi, namna ya kupata fursa za masoko na ujuzi wa kufikisha bidhaa sokoni

Amesema kuwa serikali ya Mkoa wa Morogoro ina imani kuwa wabia ambao ni Shirika la Kimataifa la CARE, SAGCOT na VETA kuwa watashirikiana kwa karibu ili kutekeleza malengo mazuri ya mradi wa UCHUMI

“Kwa upande wetu wataalamu wetu wa serikali watatumia uzoefu utakaopatikana katika mradi huu kwa manufaa ya maeneo mengine ambayo mradi huu hautafika kwa sasa kwenye ushoroba wa SAGCOT, Kongani ya Kilombelo”

Awali akizungumza katika uzinduzi huo Msimamizi wa Miradi wa CARE INTERNATIONAL Bi. Haika Mtui amesema lengo la mradi huo ni kuhakikisha linafikia vijana wasiopungua 1200 miongoni mwao ni 420 kutoka mkoa wa Morogoro ambapo hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu wawe wamefikia 164

Amesema ili kuhakikisha wanafikia lengo hilo wanafanya kazi kwa ushirikiano mkuu na wadau wengine kama SAGCOT na VETA  na kuwa mikoa ambayo inashiriki katika mradi huo ni Mbeya, Njombe na Morogoro.

Post a Comment

0 Comments