SUAMEDIA

ASA yashauriwa kujikita kuzalisha Mbegu za Alizeti ili kumaliza uhaba wa zao hilo

 



Na.Vedasto George.

Wakala wa Taifa wa Mbegu za Kilimo (ASA) wameshauriwa kujikita katika uzalishaji wa mbegu za zao la Alizeti ili kumaliza kabisa tatizo la uhaba wa mafuta ya kupikia ambayo kwa asilimia kubwa serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuagiza kutoka nje ya nchi.

Wito huo umetolewa Mkoani Morogoro na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakati ilipotembelea Wakala hao na kisha kukagua maabara ya mbegu za kilimo pamoja na ghala la kuhifadhia mbegu. 

Mwenyekiti wa kamati hiyo Dkt. Christina Ishengoma amesema Serikali ione umuhimu wa kuiwezesha ASA kutimiza majukumu yake kwa lengo la kuzalisha mbegu za kutosha kwa ajili ya wakulima.

Kwa Upande wake Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda amesema Wizara ina mpango wa kumaliza tatizo la upungufu wa mbegu kwa kushirikiana na taasisi zake zilizoko chini ya Wizara ya Kilimo ikiwemo TOSCI, ASA na TARI ili kuliwezesha Taifa kuwa na mafuta pamoja na chakula cha uhakika.

“Serikali imejipanga kuhakikisha upatikanaji wa mbegu kupitia ASA baada ya kuboresha miundombinu ya umwagiliaji katika mashamba yote yanayozalisha mbegu za kilimo”..alisema Prof. Mkenda.

Aidha Prof. Mkenda ameongeza kuwa Wizara itaongeza nguvu kwenye Taasisi ya Utafiti ya Kilimo Tanzania (TARI) ili kuwezesha utafiti wa mbegu hali itakayosaidia wakulima kupata Mbegu zenye ubora na kuhakikisha mashamba yote ya ASA yanakuwa na miundombinu ya umwagiliaji hatua inayolenga kuwezesha kupatikanaji wa mbegu bora za kilimo.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Mbegu za Kilimo (ASA) Dkt Sophia Kashenge, ameeleza changamoto mbalimbali zinazoikabili taasisi hiyo ikiwemo mgogoro wa shamba la Msimba lililopo Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro pamoja na upungufu wa maghala ya kuhifadhia mbegu zinazozalisha na ASA.

VG                                                       MWISHO




Post a Comment

0 Comments