SUAMEDIA

Wahitimu nchini watakiwa kutambua hakuna Kazi ya Maisha bali kuna Fursa za Maisha

 

Na: Catherine Mangula Ogessa

Wahitimu wa Vyuo Vikuu wametakiwa kubadili fikra zao katika karne hii ya 21 kwa kutambua kuwa kwa sasa hakuna kazi ya maisha  na badala yake waelewe kuwa kuna uhakika wa  fursa za maisha  ambazo ni nzuri na  wanatakiwa kuzidaka kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla .



Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Mhe. Jaji Mstaafu Mohamed Chande Othman, amewaasa wahitimu katika mahafali ya 36 ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA akiwataka wahitimu hao wakatumie elimu waliyoipata katika kujenga taifa lao, na wakawe wenye nidhamu na waadilifu katika kazi zao za kila siku.

…“Kwa Karne hii ya ishirini na moja, "guarantee" ni kwamba hakuna kazi ya maisha bali kuna fursa za maisha ambazo fursa nzuri nani fursa ambazo mnatakiwa mzidake,... endeleeni kupeperusha bendera ya SUA.”  Alisema Jaji Mohamed Chande Othman.

Mbali na hayo Mwenyekiti huyo wa Baraza la Chuo ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ruzuku na fedha za maendeleo inayotoa kwa Chuo, ambazo amesema ni dhahiri bila fedha hizo Chuo kisingeweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi uliofikiwa ikiwemo kuwa na idadi ya wahitimu 2943.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa  Baraza amebainisha kuwa Chuo kimeweza kutekeleza majukumu yake makuu kwa ufanisi mkubwa,  kwa  kuisimamia Menejimenti ya Chuo ili itimize majukumu makuu ya Chuo hicho ambayo ni kutoa mafunzo, kufanya utafiti, kutoa huduma za kitaalamu na ugani pamoja na kuzalisha mali.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda ameeleza kuwa, katika Mahafali ya mwaka huu 2020 Wahitimu wa Kike wameongezeka kwa asilimia 25.5, ambapo kwa mwaka huu wahitimu wa Kike ni 1097  ambao ni sawa na asilimia 37.3,  tofauti na wahitimu wa mahafali ya mwaka 2019 ambapo idadi ya wahitimu wa kike walikuwa 874.

Wahitimu hao wanatarajiwa katika kuleta  mafanikio ambayo yatakuwa  kichocheo cha ufanisi, tija na ubunifu katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa taifa ikiwemo kuzalisha mali na kutoa huduma bora kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

Katika hatua nyingine Prof. Chibunda amesema kuwa ni ukweli usiofichika kuwa  chuo cha SUA kime kuwa ni chuo ambacho kinapika wahitimu ambao kwa hakika shule wanayoipata sio ya lelemama.

 …..“Mheshimiwa Mkuu wa Chuo, Kwa kutambua kwamba kusoma na kufikia hatua ya kutunikiwa cheti katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo haijawahi kuwa lelemama niombe ridhaa yako ya kuungana na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo kuwapongeza kwa dhati watunukiwa wote kwa juhudi zao katika masomo ambazo zimewawezesha kufikia mafanikio waliyoyapata.”Alisema Prof. Chibunda

Ameongeza kuwa wanawatarajia wawe mabalozi wa kukitangaza Chuo vizuri kwa tabia na utendaji wao mzuri wa kazi, na kuwa  ni mategemeo ya Chuo kwamba watatumia elimu waliyopata kuwa wabunifu, wajasiriamali na kuzalisha ajira zao wenyewe wakijiepusha kuwa wazururaji na walalamikaji.

Akieleza kuhusu udahili kwa mwaka wa masomo 2019/2020, Prof. Chibunda amesema, chuo kimesajili jumla ya wanafunzi 5127 wapya, kati yao, 4869 ni wa  Shahada za kwanza, 151 wa shahada ya uzamili yaani wanaochukua masomo ya Umahiri na Uzamivu na kwa upande wa stashahada na astashahada ni wanafunzi 258 na  hii inafanya kuwa na idadi ya wanafunzi wapya  hadi tarehe 14 Desemba, 2020 ni 13,552.

Kwa upande wa  Kampasi Mpya ya Mizengo Pinda iliyopo katika Kijiji cha Kibaoni, Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi,  ambayo Chuo kimeanzisha, kwa mwaka huu chuo kimedahili wanafunzi 103 ambao wamesajiliwa na kuanza masomo katika katika programu tatu ambazo ni Shahada ya kwanza ya Sayansi ya Usimamizi Rasilimali Nyuki (BSc. Bee Resources Management), Stashahada ya Uzalishaji na Usimamizi wa Mimea Vipando (Diploma in Crop Production and Management) na Astashahada ya Uongozaji Watalii na Uwindaji Salama (Certificate in Tour Guiding and Hunting Operations).

KATIKA PICHA 


KATIKA VIDEO BOFYA HAPA CHINI



Post a Comment

0 Comments