SUAMEDIA

SUA yatakiwa kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa vitendo ikiwemo kuboresha mitaala yake

 

Na.Vedasto George.

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimetakiwa kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa vitendo  ikiwemo kuboresha mitaala yake ya ufundishaji  ili kuwafanya wanafunzi wanaohitimu katika chuo hicho kujiajiri na kuajiri wengine.



Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Idara ya  Sayansi Teknolojia na   Ubunifu kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Maulilio  Kipanyula  ambaye amemwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Tekinolojia Dkt. Reonald Akwilapo  katika halfa ya kutoa zawadi kwa wanafunzi wahitimu SUA na kusema umefika muda muafaka kwa chuo kuangalia mitaala inayotumika kufundishia ili iweze kulenga zaidi kwenye kujiajiri.

“Ni wakati muafaka sasa kupunguza idadi ya wahitimu ambao wanamaliza na kwenda tu kutafuta kazi, mitaala lazima iwawezeshe wahitimu wanapo kwenda huko duniani  waweze kujitegemea na kuzalisha ajira” alisema  Prof. Maulilio  Kipanyula. 

Prof. Kipanyula ameongeza kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuvisaidia vyuo vikuu nchini viweze kuendelea kuzalisha wataalamu ambao wataweza kulisaidia taifa katika sekta mbalimbali ikiwemo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphaeli Chibunda amesema  wanafunzi waliofanya vizuri na kupewa zawadi ni 211 ambao wametoka katika Ndaki na Shule mbalimbali chuoni hapo ikiwemo wanafunzi bora wa mwaka ambao ni 195 pamoja na Idara sita bora ambazo zimefanya vizuri  kwa kuchapisha katika tovuti

Prof. Chibunda amesema chuo kitaendelea kutoa zawadi kwa wanafunzi wahitimu waliofanya  vizuri  kila mwaka katika masomo ili kutambua jitihada  za makusudi zinafanywa na wanafunzi hao huku akisema hiyo ni motisha ili wengine nao wafanye vizuri zaidi.

Nao  baadhi ya wanafunzi ambao wamefanya vizuri katika masomo yao akiwemo Idi Msangi na Upendo Nzaligo wamesema jitihada na kujituma ndiyo chachu ya mafanikio waliyoyapata.

“Nashukuru mwenyezi Mungu najua ni hatuma moja nimeipiga kwenda mbele masomo yalikuwa magumu ila ni kwa uwezo wake Mungu nimekuwa miongoni mwa wanafunzi  bora wa mwaka, nawashauri wanafunzi wenzangu tunapokuwa shule tusome kwa bidii zaidi” alisema Idi Msangi




 

Post a Comment

0 Comments