Na:Tatyana Celestine
Watumishi wa Umma wakiwemo wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA wametakiwa kujua kwa undani Sheria za Utumishi wa Umma, Sheria na Kanuni za Usimamizi wa Fedha na Mali, Sheria za Kazi, Sheria za Ununuzi wa Umma na Utunzaji wa Nyaraka na Siri za Ofisi.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Mkuu wa
Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda leo 21 Octoba, 2020 wakati akifungua mafunzo
ya Dhana ya Uadilifu na Nafasi ya Uongozi katika Utendaji na Ufanisi wa Taasisi
za Umma Nchini kwa wafanyakazi viongozi wa SUA.
Chibunda amesema kuwa mafunzo hayo ni
muhimu yakiwa chachu kwa viongozi mbalimbali wa chuo hicho katika mambo muhimu
ikiwemo maadili ya utumishi wa umma ambayo yatamsaidia kiongozi kutambua yeye
ni mtu wa kwanza katika kuonesha mfano kwa anaowaongoza.
Aidha amewataka viongozi hao kujitoa
kushiriki kikamilifu ili kuweza kupata maarifa ambayo yatawajenga kwa manufaa
ya sasa na baadae kwani mafunzo hayo ni mwanzo wa umahiri katika kazi.
Nae mtoa mada katika mafunzo hayo
Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Maadili Kazini kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti
ya Utumishi wa Umma Bw. Fabian Pokela amewakumbusha viongozi hao kuwa mashirika
yote ya Umma nchini yamekasimiwa majukumu ili kufikia malengo ya taasisi zao
ikiwemo SUA, hivyo Serikali inategemea kuona matokeo chanya yatokanayo na
taasisi hizo katika utendaji kazi
Aidha Pokela amemtaja Rais wa Awamu ya
Tano Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kama mfano kwani alipoingia madarakani na
jambo la kwanza kulishughulikia likawa ni uadilifu serikalini hivyo SUA
inapaswa kuiga mfano huo ili kuweza kufikia malengo iliyojiwekea.
Amesema kuwa katika kufikia malengo
lazima kuwe na vipaumbele ambavyo vinawekwa na taasisi pamoja na taifa kitu
ambacho wengi wanasahau na kufanya taasisi nyingi kutofikia malengo
waliyojiwekea kwa kukosa uadilifu.
Akizungumzia suala la sheria amesema
kuwa viongozi wanatakiwa kufuata sheria na kanuni zilizowekwa ili kuweza
kumsaidia kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kusema kuwa ili viongozi
waweze kutambua nafasi zao za uongozi ili kuweza kutatua changamoto zinazojitokeza
katika maeneo yao ya kazi.
Mafunzo hayo ya Dhana ya Uadilifu na
Nafasi ya Uongozi katika Utendaji na Ufanisi wa Taasisi za Umma nchini
ambayo yameandaliwa na SUA kwa watumishi viongozi wa Taasisi hiyo yameanza leo
21/10/2020 hadi 23/10/2020 na yamejumuisha Marasi wa Ndaki, Amidi wa Shule Kuu
na wakurugenzi Taasisi na Vitivo, Naibu Rasi wa Ndaki, Naibu Amidi wa Shule Kuu
na Makatibu, Wakuu wa Idara za Taaluma na Utawala na Wakuu wa
Idara.
Baadhi ya Viongozi walioudhuri mafunzo ya Dhana ya Uadilifu na Nafasi ya Uongozi katika Utendaji na Ufanisi wa Taasisi za Umma nchini. |
Baadhi ya Viongozi walioudhuri mafunzo ya Dhana ya Uadilifu na Nafasi ya Uongozi katika Utendaji na Ufanisi wa Taasisi za Umma nchini. |
0 Comments