SUAMEDIA

SUA kuhakikisha Kilimo Ikolojia kinakuwa endelevu

 Na Farida Mkongwe         SUA - Morogoro

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kimesema kinaendelea kushirikiana na Wakulima na Wadau wengine wa kilimo katika kuhakikisha Kilimo Ikolojia kinakuwa endelevu kwa kuwa ni kilimo chenye tija na kinachozingatia utunzaji wa mazingira.



Hayo yamebainishwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Utawala na Fedha kutoka SUA Prof. Amandus Muhairwa kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda wakati akifungua Mdahalo wa  Siku ya Chakula Duniani ambao umefanyika chuoni hapo kwenye Kampasi ya Edward Moringe mjini Morogoro

Prof. Muhairwa amesema katika kuhakikisha Kilimo Ikolojia kinakuwa endelevu Chuo kimeanzisha Shahada ya Kilimo cha Ikolojia ili kuweza kuzalisha wataalam watakaoendeleza kilimo hicho.



Awali akizungumza katika Mdahalo huo  Cecile Frobert kutoka Ubalozi wa Ufaransa amesema Ufaransa na wadau wengine wa kilimo  inaendelea na juhudi za kuendeleza Kilimo Ikolojia ambacho kinasaidia kukifanya kilimo kuwa endelevu huku akitoa wito wa kuepukana na kilimo cha mazoea cha kutumia madawa ambacho kina madhara kiafya.

Kwa upande wake Jasmien De Winne kutoka Ubalozi wa Ubeligiji amesema vipaumbele vya nchi hiyo ni kufanya shughuli endelevu za kilimo zinazolenga kuboresha maisha ya watu  na kuwataka wadau wa Kilimo kujifunza kuendeleza kilimo ambacho hakitaharibu mazingira na kitakuwa na faida kwa kizazi cha sasa na kijacho

Akizungumzia mdahalo huo Mratibu wa Kituo cha Kilimo Ikolojia ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza ICE- SUA Prof. Dismas Mwaseba amesema kwa muda sasa Chuo kimekuwa kikifanya tafiti zinazolenga kumuwezesha mkulima kupata zaidi bila kuharibu mazingira 

Kwa upande wao baadhi ya wakulima walioshiriki katika Mdahalo huo akiwemo Msakuzi Idd na Bahati Swalehe kutoka kata ya Mbuyuni kijiji cha Kibwaya kilichopo Morogoro vijijini wamesema tangu walipoanza kutumia Kilimo Ikolojia wameweza kupunguza gharama za kilimo na hivyo kupata faida zaidi.

Mdahalo huo wa siku moja ambao umehusisha wadau kutoka SUA , SAT, RECODA, Wakulima,Wanafunzi  pamoja na Wadau wengine wa Kilimo  umebeba kauli mbiu isemayo "Kilimo cha Ikolojia kama njia ya kuelekea Mfumo Endelevu wa Chakula".






Post a Comment

0 Comments