Na.Vedasto George, Morogoro
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na
Biashara Prof. Riziki Shemdoe amewataka watafiti nchini kufanya tafiti zitakazosaidia kutumia rasilimali za ndani
kwa ajili ya maendeleo endelevu ya
uchumi wa viwanda.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe akizungumza na washiriki wa mdahalo hawako pichani katika ukumbi wa Freedom Square Mazimbu
Akizungumza katika mdahalo wa
wazi wa uchambuzi wa matokeo ya tafiti katika utunzi wa sera na mipango ya
maendeleo uliyoandaliwa na Mradi wa Uwezeshaji
na Uhishaji wa Matumizi ya Matokeo ya Tafiti
katika Uundaji wa Sera na Mipango
ya Maendeleo nchini uliopo chini ya Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo SUA Prof. Shemdoe
amesema ukuaji wa uchumi unategemea
tafiti mbalimbali zinazofanywa na watafiti wa ndani.
Pia Prof. Shemdoe ameongeza kuwa
tafiti nyingi zinazofanywa nchini zimekuwa zikiishia kwenye majarida na
makabati bila ya kuleta manufaa kama inavyotegemewa.
“Pamoja na serikali kutumia matokeo ya tafiti kutunga sera na mipango ya maendeleo nchini, bado matokeo ya matumizi ya tafiti hizo siyo wa kuridhisha, matokeo mengi ya tafiti na taarifa za kitaalamu zinaishia kwenye majarida na makabati na ofisi tu”. Alisema Prof. Shemdoe.
Aidha Prof. Shemdoe ameongeza
kuwa mpango wa maendeleo ya serikali wa miaka mitano kuanzia 2016 mpaka 2021
umejikita katika kuhakikisha kuwa kunakuwa na muunganiko wa uwezo wa ndani wa sayansi,
teknolojia na uvumbuzi kupitia uwekezaji katika mtaji wa rasilimali watu,
taasisi na kuboresha mifumo ya uvumbuzi nchini.
“Ukamilifu na utekelezaji wa ajenda ya mwaka 2030 hasa katika nchi zinazoendelea unategemea sana uwekezaji katika tafiti za kisayansi, teknolojia, ubunifu na uvumbuzi kwa kuzingatia mahitaji yetu kwa uhalisia wake”, alisema Prof.Shemdoe
Mratibu wa Mradi wa kuongeza uwezo wa tafiti
kusanisi matokeo ya tafiti Dr.Faith
Mabiki amesema lengo la mradi huo ni kuchangia katika juhudi
za serikali ili kuongeza uwezo wa
watafiti kusanisi matokeo ya
tafiti ili ziweze kutumika katika maamuzi mbalimbali ya kisera kwa maendeleo ya Taifa.
Hata hivyo Dkt. Mabiki amesema mradi
huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa idara mbili ambazo ni Idara ya Kemia na
Fizikia pamoja na Idara ya Sera, Mipango na Menejimenti ya Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia
Akisoma Hotuba ya Makamu wa Mkuu
wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA, Naibu Makamu mkuu wa chuo hicho
upande wa Taaluma Prof. Maulid Mwatawala
amesema Bara la Afrika lipo nyuma katika utoaji wa matokeo ya tafiti licha ya
kuwa na idadi kubwa ya watu.
Prof. Mwatawala ameongeza
kuwa taarifa ya Shirika la Elimu, Sayansi
na Utamaduni la Umoja wa Mataifa
(UNESCO) ya mwaka 2015 inaonesha kuwa bara la Afrika linazalisha asilimia 2.6
ya tafiti duniani huku bara hilo likiwa linachangia asilima 2.9 ya watafiti
wote duniani.
“ Takwimu hizi ni wazi kuwa uchangiaji wa tafiti kwa maendeleo ya bara la Afrika na Tanzania ni mdogo” amesema Prof Mwatawala.Naibu Makamu mkuu wa chuo hicho upande wa Taaluma Prof. Maulid Mwatawala akitoa hotuba yake
Mratibu wa Mradi wa kuongeza uwezo wa tafiti kusanisi matokeo ya tafiti Dr.Faith Mabiki akizungumza katika mdahalo huo
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe katikati aliyevaa miwani akiwa na viongozi kutoka vyuo mbalimbali
0 Comments