SUAMEDIA

Watanzania wametakiwa kujenga utamaduni wa kupenda kusoma machapisho hasa yahusuyo kilimo

Na: Farida Mkongwe

Watanzania wametakiwa kujenga utamaduni wa kupenda kusoma machapisho mbalimbali hasa yahusuyo kilimo ili waweze kuzalisha mazao kwa wingi na yenye ubora ambao unakubalika ndani na nje ya nchi.



Wito huo umetolewa na Mwalimu Mustapha Sultani ambaye pia ni Mkutubi katika Maktaba ya Taifa ya Sokoine ya Kilimo SNAL wakati akizungumza na SUAMEDIA kuhusu umuhimu wa wakulima kujifunza kupitia machapisho yanayotolewa na maktaba hiyo.

Mwalimu Sultani amesema SNAL ina kitengo kinachojulikana kwa jina la Ghala la Machapisho kwa Mkulima ambacho kinatoa habari na taarifa za kilimo kwa ajili ya matumizi ya wakulima nchini lakini wakulima wengi bado hawana mwamko wa kujisomea ili kujiendeleza.

“Habari na taarifa zilizopo katika kitengo hiki cha Ghala la machapisho kwa mkulima zinatokana na taarifa na tafiti mbalimbali zilizofanywa na wataalamu wa kilimo wa SUA na taasisi nyingine za kilimo ndani na nje ya nchi hivyo zina manufaa makubwa kwa wakulima, kitu muhimu ni wakulima kutenga muda wao na kuyasoma”, alisema Mkutubi huyo.

Aidha mwalimu Sultani amewataka wakulima kuacha tabia ya kulima kwa mazoea na badala yake watumie teknolojia za kisasa ambapo elimu ya ziada na kiada kuhusu kilimo bora wataipata kwenye machapisho hayo yanayotolewa na kitengo hicho cha Ghala la Machapisho kwa Mkulima kichopo Maktaba ya Taifa ya Sokoine ya kilimo.

“Kwa wale wakazi wa Morogoro wanaweza kuja moja kwa moja pale SUA na kupata elimu hii lakini kwa walio mbali na wasioweza kupata nafasi basi wanaweza kuingia kwenye tovuti yetu www.lib.sua.ac.tz ambapo kuna kiunganishi chenye jina Mkulima Collection au unaweza kwenda https://www.lib.sua.ac.tz ukazipata taarifa zetu”, alifafanua Mwalimu Sultani.




Post a Comment

0 Comments