SUAMEDIA

Wamama na vijana kunufaika na mafunzo ya biashara ili kuongeza uzalishaji



Na Gerald Lwomile

Bariadi

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent  Bashungwa amewaagiza Makatibu Wakuu wa Viwanda, Biashara na Kilimo kuhakikisha kina mama na vijana wanapata huduma ya mafunzo ya biashara kwenye shughuli za uzalishaji ili wapate tija

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa akitoa hotuba yake kwenye kongamano (Picha zote na Gerald Lwomile)

Akizungumza leo Agosti 5, 2020 katika kongamano lililoandaliwa na Jumuiya ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania katika maonesho ya wakulima Nanenane katika viwanja vya Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu Waziri huyo wa Viwanda na Biashara amesema kama kina mama watapata huduma ya mafunzo ya biashara basi kutakuwa na maendeleo makubwa katika biashara zao

“Sasa naagiza kwa Katibu wetu wa Viwanda na Biashara na Katibu Mkuu wa wizara ya kilimo mkakati wetu wa kufungamanisha kilimo na viwanda, hakikisheni wataalamu wetu wa kliniki ya huduma wanafanyakazi ipasavyo, wanatembea kwenye mikoa na hawakai ofisini ili kuwahudumia kinamama hawa”, amesema Mh. Bashungwa

Amesema zipo fursa nyingi ambazo kina mama wanaweza kuzitumia na zikawaletea maendeleo kama wataendelea kutimiza wajibu wao kwa kufanya kazi kwa bidii kama wanavyofanya sasa

Katika hatua nyingine Mhe. Bashungwa amesema kama mfuko wa kusaidia kina mama ulioanzishwa na benki ya Azania kwa kushirikiana na Shirika la Taifa la Hifadhi  ya Jamii ambapo zaidi ya shilingi bilioni 5 zimetolewa ili kusaidia kina mama kwa kupata mikopo nafuu
Wakinamama wajasiliamali wakimsikiliza waziri wa Viwanda na Biashara hayupo pichani wakati wa kongamano

Amesema serikali inaendelea na mazungumzo na taasisi zingine za kifedha kutenga fedha kiasi kwa ajili ya mfuko huo ambao una lengo la kuwasaidia kina mama na vijana wajasiliamali

Awali akitoa taarifa kwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Wanawake Wafanyabiashara Bibi. Doreen Mawala amesema Jumuiya hiyo ina lengo la kuwawezesha kinamama kiuchumi kwa kutumia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kongamano kama hilo

Amesema mbali na kutoa mafunzo mbalimbali lakini pia wamekuwa wakitafuta masoko ya bidhaa za kinamama na kuwaunganisha na masoko kwa kutumia maonesho ya kilimo

Post a Comment

0 Comments