Na: Farida Mkongwe, Dar es Salaam
Wanafunzi wanaotaka kujiunga na vyuo vikuu wametakiwa kufika
katika banda la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA lililopo kwenye Maonesho
ya Vyuo Vikuu yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar Es Salaam
ili waweze kupata ushauri na udahili wa kujiunga na chuo hicho.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Ugani cha Taasisi ya
Elimu ya Kujiendeleza ICE kilichopo SUA Dkt. Innocent Babili ambaye ni Mratibu
wa Maonesho ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia upande wa SUA wakati
akizungumza na SUAMEDIA katika maonesho hayo.
Dkt. Babil amesema maandalizi yote kwa ujumla yamekamilika na
kwamba wananchi watakaofika katika banda hilo la SUA hususan wanafunzi
wanaotaka kujiunga na vyuo vikuu ambao ndio walengwa wakifika watajionea
teknolojia mbalimbali zilizopo SUA sanjari na kudahiliwa kwa wale waliokidhi
vigezo.
“Lengo kubwa hapa ni kuwasaidia vijana waliomaliza kidato cha
sita ambao wanataka kujiunga na vyuo vikuu, hapa kuna fursa ya kuweza kupata
udahili wa moja kwa moja lakini pia watapata ushauri wa kozi zilizopo na faida
zake katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia”, alisema Dkt. Babil
Maonesho hayo ya wiki moja ya Elimu ya Juu, Sayansi na
Teknolojia ambayo yamebeba kauli mbiu isemayo “ Nafasi ya Elimu ya juu katika
kuleta mabadiliko ya kiuchumi na maendeleo endelevu”, yameanza rasmi leo Agosti
31 na yatakamilika Septemba 5 mwaka huu.
0 Comments