Na : Gerald Lwomile
Inakadiriwa kuwa mwaka 2020 zaidi ya watoto 440,000 walio chini ya umri wa chini ya miaka mitano wataathirika na utapiamlo mkali licha kuwepo kwa viashiria vya kupungua kwa udumavu kwa watoto walio chini ya miaka 5
Haya yamesemwa leo Agosti 27, 2020 na Waziri wa Afya
na Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu katika hotuba yake
iliyosomwa na Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara hiyo, Bw. Edward
Mbanga wakati akizindua mradi wa kutengeneza vyakula vya nyongeza kwa watoto
wenye umri chini ya miaka 5
Mbanga amesema idadi ya watoto waliodumaa imeongezeka
kutoka milioni 2.7 mwaka 2014 hadi kufikia milioni 3 mwaka 2018 kutokana na
ongezeko la jumla ya idadi ya watu
“Ulishaji sahihi wa watoto wakiwemo watoto wachanga umekuwa
chini sana, ambapo mnamo mwaka 2018, asilimia 58 ya watoto wachanga wenye umri
wa miezi 0-5 waliripotiwa kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee, asilimia 35 ya
watoto wenye umri wa miezi 6-23 walipatiwa vyakula mchanganyiko kwa kiasi
kidogo na asilimia 30 walipata kiwango cha chini cha chakula kilichokidhi
mahitaji ya mtoto|”
Mkurugenzi huyo ameendelea kusema kuwa katika
kupambana na utapiamlo Serikali imekuwa ikitekeleza mpango mkakati wa Kitaifa
wa Lishe ulioanza mwaka 2016 na unatarajia kufikia tamati 2021 ambao umejikita
katika kuhakikisha watoto, wanawake, na wanaume wanapata lishe bora na kuondoa
utapiamlo, ukondefu na udumavu
Akitoa wasilisho lake katika uzinduzi huo Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Dkt. German Leyna amesema pamoja na kuwa
Tanzania imeonyesha mafanikio katika jitihada za kuondoa udumavu, ukondefu na
uzito uliopungua bado haijafikia malengo ya kidunia
Akitoa salamu za Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA
kwa niaba ya Makamu Mkuu Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael
Chibunda, Naibu wa Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA
upande wa Taaluma Prof. Maulid Mwatawala
amesema SUA itashirikiana na Serikali katika kuhakikisha mradi huo unafanikiwa
Katika Mradi huo SUA kupitia Idara ya Teknolojia ya Chakula, Lishe na Sayansi za Walaji inatarajiwa kutengeneza vyakula hivyo vya nyongeza kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano
MATUKIO KATIKA PICHA
Mkuu wa Kitengo cha Sayansi ya Chakula kutoka Chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine Dk. Rashid Juma akiwaonyesha wadau wa lishe (hawapo pichani) mfano wa unga utakaotumika kuzalishia Chakula cha nyongeza, katika mradi wa kutengeneza vyakula vya nyongeza kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano, ambao umezinduliwa Mkoani Morogoro na utatekelezwa na TFNC,MUHAS, SUA NA TBS kupitia ufadhili wa WFP.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili Prof. Andrea Pembe akisikiliza maelezo ya namna vyakula vya nyongeza kwa Watoto chini ya Umri wa miaka mitano vitakavyoandaliwa, kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Sayansi ya Chakula wa Chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine Dk. Rashid Juma wakati wa uzinduzi wa mradi huo.
Baadhi ya Viongozi wa Taasisi zinazoshiriki kwenye mradi wa kutengeneza vyakula vya nyongeza kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, wakiangalia mojawapo ya mashine ambayo itatumika katika uzalishaji wa vyakula hivyo, mara baada ya kutembelea eneo la kiwanda kitachotumika kuzalisha malighafi zitakazotumika kuandalia vyakula hivyo vya nyongeza, katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
0 Comments