Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. John Pombe Magufuli leo amewaongoza viongozi mbalimbali kuuaga mwili wa Hayati Benjamin Wiliam Mkapa na kusema kuwa dunia imepoteza kiongozi ambaye alikuwa ni hazina ya dunia.

Akizungumza wakati akilihutubia taifa Rais Magufuli amesema hayati Mkapa alikuwa ni kiongozi muadilifu, mchamungu, jasiri, mwanadiplomasia, mzalendo, na mpenda amani na utulivu na kwamba dunia itamkumbuka daima.
Katika hatua nyingine Rais Magufuli ametangaza rasmi kuwa uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam sasa utaitwa uwanja wa Benjamin Mkapa kwa lengo la muenzi kiongozi huyo ambaye pia alitoa mchango mkubwa kwenye sekta ya michezo na pia ndiye aliyehusika katika ujenzi wa uwanja huo.
"Mzee Mkapa aliujenga uwanja mkubwa wa michezo, kwa sasa wengi wanataka uwanja uitwe Mkapa Stadium, Mzee Mkapa alikuwa hapendi vitu viitwe kwa jina lake, lakini kwa kuwa hawezi kuniadhibu chochote amelala hapo, natamka rasmi uwanja uitwe Mkapa Stadium", amesema Dkt. Magufuli.
Akielezea zaidi namna ambavyo watanzania wataendelea kumkumbuka Hayati Benjamin Mkapa, Dkt. Magufuli amesema kiongozi huyo alichukia rushwa, alisimamia misingi ya ukweli na uwazi, alileta mageuzi katika sekta ya elimu, na aliamini maendeleo kuwa ndio njia pekee na chachu ya kukuza uchumi wa nchi.
"Watanzania wanamkumbuka Mh. Mkapa kwa mageuzi ya uchumi, wakati anaingia madarakani nchi yetu ilikuwa na matatizo ya kiuchumi, na wakati huo alianza kulipa madeni na kuanza kuzishawishi taasisi za kifedha pamoja na nchi wahisani kufuta madeni", alielezea Rais Magufuli.
Hayati Benjamini Wiliam Mkapa ambaye alikuwa Rais wa awamu ya tatu wa Tanzania alifariki dunia Julai 23 mwaka huu na atazikwa kesho siku ya Jumatano Julai 29 kijijini kwake Lupaso wilayani Masasi mkoani Mtwara.
Zaidi kwenye video hapa chini
0 Comments