SUAMEDIA

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, SUA kimeingia mkataba wa makubaliano ya
ushirikiano (MoU) na Chuo Kikuu cha Greenwich cha Uingereza kupitia programu
ya Mpango wa Usalama wa Chakula na Lishe (FaNSI) ya Taasisi ya Maliasili (NRI).

Makubaliano hayo yaliyofanyika Kampasi Kuu ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo tarehe 16 Oktoba 2019 yalitanguliwa na uwasilishwaji wa taarifa na historia
fupi za vyuo hivyo viwili.

Lengo la makubaliano hayo ni kushirikiana katika Nyanja mbalimbali ikiwemo
katika Shahada za Uzamivu na kubadilishana uzoefu wa namna ya kuandika
maandiko ya mapendekezo huku Kituo cha Kudhibiti wa Viumbe hai waharibifu
kutoka SUA kikiwa moja ya wadau pekee wa program hiyo katika Nchi za kusini
wa Jangwa la Sahara.

Kupitia makubaliano hayo Mwanataaluma mmoja wa SUA amefanikiwa kupata
ufadhili wa shahada ya uzamivu kwenda kusoma na kujifunza katika Chuo Kikuu
cha Greenwich Januari 2020.

Mkurugenzi wa Kituo cha Kudhibiti wa Viumbe hai waharibifu, Dkt. Ladislaus
Mnyone amekipongeza Chuo kikuu hicho cha Greenwich kwa kufanikisha swala
hilo ambalo litaleta tija baina ya vyuo vyote viwili.

Dkt. Mnyone amewashauri wanafunzi kuchangamkia fursa hiyo hasa kwenye
upande wa tafiti ambazo zinazoweza kutatua changamoto mbalimbali Tanzania na
duniani kwa ujumla.

NRI ni taasisi iliyobobea kwenye tafiti za maendeleo ya kijamii kama Chakula,
Kilimo, Mazingira na Maisha Endelevu ambayo inasimamia programu ya Mpango
wa Usalama wa Chakula na Lishe (FaNSI) ili kutatua changamoto zinazolikumba
bara la Afrika hasa kwenye upatikanaji wa mlo kamili.

Chuo Kikuu cha Greenwich kupitia FaNSI kinafanya kazi na taasisi mbalimbali
barani Afrika ambapo Chuo Kikuu cha Sokine cha Kilimo, SUA ikiwa ni moja ya
taasisi hizo kwa sasa.

Post a Comment

0 Comments