Uongozi wa Kiwada cha kusindika maziwa cha Tanga Fresh kimewashauri wafugaji Kanda ya Mashariki na Tanzania kwa Ujumla kutumia matokeo ya tafiti mbalimbali za kisayansi za ufugaji wa Ng'ombe wa maziwa ili kuongeza tija.
Wito huo umetolewa na Meneja Vyanzo vya maziwa wa kiwanda hicho Bi. Nadomana Nyanga wakati akiongea na Waandishi wa habari wa Kanda ya Mashariki na watafiti waliokuwa kwenye mafunzo kwa vitendo mafunzo ya namna ya kuandika habari za Sayansi,Teknolojia na ubunifu yaliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).
Bi.Nyanga amesema kiwanda hicho kinauwezo wa kusindika lita 120,000 kwa siku lakini wanapata maziwa lita 30,000 hadi 50,000 za maziwa kwa siku,kiwango kisichokidhi mahitaji kutokana na uwezo mdogo wa ng'ombe kutoa maziwa.
Amesema sayansi ndio njia pekee ambayo ikitumiwa vizuri inaweza kusaidia kuongeza uzalishaji wa maziwa kwa kiasi kikubwa na hivyo kuondoa pengo kubwa la ukosefu wa maziwa huo ambao unapelekea wao kufuata maziwa kwenye mikoa mbalimbali ya nje ya Kanda ya mashariki hasa katika wakati wa kiangazi ambapo malisho huwa ya tabu.
Meneja huyo wa Vyanzo vya maziwa ameongeza kuwa wao kama kiwanda wanashirikiana na Taasisi ya Utafiti wa mifugo Tanzania TALIRI katika kuhakikisha wanapata malisho bora yaliyofanyiwa utafiti pamoja na aina bora za ng'ombe wanaotoa maziwa mengi tofauti na hawa wa asili.
“Ng'ombe wanapopitia kwenye mahangiko yaani (stress) wanapoteza uwezo wao wa kutoa maziwa bora hivyo ni muhimu wafugaji wakatumia ushauri wa watafiti katika kuhakikisha wanasimamia mahitaji muhimu ya mifugo hasa malisho,maji na afya" Alisisitiza Bi. Nadomana Nyanga.
Amebainisha kuwa pia kiwanda kinahamaisha unywaji wa maziwa kwa watanzania kutoka na jamii kutokuwa na muamko wa unywaji maziwa kwani kwa Tanzania mtu mmoja anakunywa watstani wa lita 47 kwa mwaka wakati wenzetu majirani Wakenya mtu anakunywa lita 100 kwa mwaka hivyo ili kufikia huko lazima hamasa itolewe kwa jamii lakini pia uzalishaji uongezeke.
Katika hatua nyingine katika kuongeza maslahi na ubora wa maziwa amesema kiwanfa hicho cha Tanga fresh kinataka kuanzisha utaratibu wa kuwalipa wafugaji bei kutokana na ubora wa maziwa wanayozalisha kama nchi zingine duniani zinavyofanya.
"Zimbabwe wanawalipa wafugaji kwa kutokana na ubora wa maziwa hivyo sisi kama viongozi wa sekta kwenye maziwa nchini tunaona tuanze kufanya hivyo pia ili kuwahamasisha wafugaji kuzingatia mbinu bora za ufugaji ili ng'ombe wao watoe maziwa bora na yenye viwango” Alisisitiza Bi. Nyanga.
Akizungumzia changamoto hiyo ya uchache wa maziwa,tatizo la malisho Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya utafiti wa mifugo Tanzania ofisi ya Kanda ya Mashariki Dkt. Zabron Nziku amesema malisho duni ndio sababu ya uzalishaji mdogo wa maziwa kwa mifugo hivyo kituo chake kinafanya utafiti wa malisho bora ambayo wafugaji wakiyatumia yatasaidia kuongeza uzalishaji na kipato.
Amesema tayari wanazo aina mbalimbali za malisho ya mifugo ambayo wanayafanyia utafiti katika kituo chake na yameonyesha kufanya vizuri lakini yapo ambayo tayari wafugaji wameshaanza kuyatumia kuwalisha mifugo yao baada ya kazi kubwa ya kukusanya aina bora za malisho nchi nzima na kuyachambua.
Dkt. Nziku amesema pamoja na malisho pia wanazo teknolojia rahisi za utunzaji wa malisho am,bazo wanawashauri wafugaji kuzitumia ili kuhifadhi malisho kwaajili ya kiangazi ambapo kunakuwa na uhaba wa malisho na kusababisha kushuka kwa uzalishaji wa maziwa.
"Tuna wafugaji ambao sasa wanatenga maeneo makubwa sana kwaajili ya kuzalisha chakula bora cha mifugo na kwakweli mahitaji ni makubwa sana hivyo niwashauri watanzania kuingia kwenye kilimo cha malisho ya mifugo maana soko lipo ndani nan je ya nchi” Alisistiza Dkt. Nziku.
0 Comments