SUAMEDIA

Mhe. George Simbachawene awapongeza Watafiti wa SUA kwa kusimamia Afya ya Vyura wa Kihansi

Na: Calvin E. Gwabara
Waziri wa nchi  Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Maizngira Mhe. George
Simbachawene amepongeza kazi kubwa inayofanywa na watafiti wa Chuo Kikuu
cha Sokoine cha Kilimo (SUA)  katika kuhakikisha vyura wa Kihansi wanaendelea
kuhifadhiwa pamoja na Biyoanuai zote zilizopo katika eneo hilo la Kihansi.
Prof. Gerald Misinzo (kushoto) akitoa maelezo kwa Mhe. George Simbachawene (kulia) na Prof. Raphael Chibunda (katikati) wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) alipotembelea Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
Ametoa pongezi hizo wakati wa ziara yake chuoni hapo na kupata taarifa ya kazi zinazofanywa na watafiti wa SUA kwa kushirikiana na wadau wengine katika kulinda mazingira na viumbe katika eneo hilo la bwawa la kihansi kabla ya kutembelea kuona hali halisi katika eneo hilo.

Mhe. Simbachawene ambaye ameambatana na Mwenyekiti wa bodi ya NEMC
nawataalamu wengine kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam na wizara yake
amesema swala kubwa linalopaswa kuzingatiwa katika kazi hiyo ni kuhakiksha
zinapatikana njia endelevu za kutunza bayoanuai zote katika eneo hilo la Kihansi
badala yakufikiria kutumia fedha nyingi katika kutunza vyura peke yake.

Amewataka wataalamu hao wote wanaoshiriki katika kulinda na kutunza eneo hilo
kukaa pamoja na kutengeneza andiko ambalo litaonyesha faida kwa ujumla za
utunzaji wa eneo hilo hasa nafasi ya utalii kwa watu mbalimbali wanapenda kuja
kuangalia vyura hao ambao hawapatikani kokote duniani.

Katika hatua nyingine amewaagiza Wataalamu wa NEMC na ofisi yake kuhakikisha
wanaanza mchakato wa kupata haki miliki ya uvumbuzi na utafiti wa kahawa pori
ya Kihansi ambayo imeonekana kuwa na ubora mkubwa ikilinganishwa na aina ya
  Arabika na Robusta ili nchi iweze kupata haki yake kabla ya watafiti wa nchi
nyingine kuwahi kwakuwa wanaona machapisho mbalimbali ya watafiti hao
wanayoyafanya.

Awali akiwasilisha mada fupi kuhusu kazi zinazofanywa na SUA katika utunzaji wa
Vyura hao Prof. Gerald Misinzo amesema walianza kazi hiyo muda mrefu mara
baada ya kugundulika kuwa idadi ya vyura hao wanatoweka na baadae Serikali
kuamua kwenda kuwahifadhi nje ya nchi na baada ya muda vyura hao
wamerudishwa nchini na kuzalishwa katika Chuo Kikuu cha Dar es salaamu
ambapo wameanza kurudishwa taratibu katika eneo la Kihansi.

Dkt. Misinzo amesema kazi kubwa ambayo wataalamu wa SUA wamekabidhiwa
ni kuhakikisha wanaangalia magonjwa na tiba za magonjwa kwa vyura ili
wasiendelee kuathiriwa na kubainisha kuwa tatizo kubwa ambalo wameligundua
ni  magonjwa ya fangasi hivyo jitihada zinaendelea kuhakikisha wanatokomeza
magonjwa hayo.
Kwa upande wake Prof. Paul Kusolwa Mtaalamu wa Uzalishaji wa Mimea kutoka
Ndaki ya Kilimo akiwasilisha fursa nyingine ambazo pia wao kama watafiti
wameiona na uwepo wa aina ya kahawa pori ambayo baada ya kuifanyia utafiti
kwa muda mrefu wanaona inaweza kuwa ya kipekee kutokana na kuwa na sifa
nzuri ikilinganishwa na hizi zilizopo kwa sasa.

Amesema tayari wameshafanya utafiti wa kina na kupata matokeo mazuri hivyo
wamewakabidhi Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TACRI) ili waweze kuendelea
wakizingatia kuwa mradi huo ufadhili wake unafikia mwisho na ni lazima utafiti
huo uendelee ili uweze kuzalisha kahawa.
Akishukuru kwa ujio wa Waziri huyo Makamu wa Mkuu wa Chuo Prof. Raphael
Chibunda amemuomba Waziri Simbachawene na Wataalamu wa NEMC kuona
umuhimu wa kuwezesha Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kupata maabara
maalumu ambayo itakuwa na uwezo wa kufanya tafiti zote zinazohusu masuala ya
mazingira nchini ikizingatiwa kuwa SUA inao wataalamu wengi wabobevu katika
Nyanja hiyo.
Amesema hivi sasa wataalamu hao wanafanya tafiti zinazohusu masula ya mazingira
kwenye maabara ambazo sio maalumu kwa kazi hiyo na kujikuta wanachanganyika
na watafiti wa masuala mengine mbalimbali ikiwemo kilimo hali ambayo inaweza
kushusha ufanisi katika kufanya tafiti na kupata majibu ambayo yataleta tija kwa
Taifa.
Prof. Chibunda amemhakikishia Waziri Simbachawene kuwa chuo kipo tayari
kushirikiana na ofisi yake na ofisini zingine katika kuanzisha maabara hiyo na
kufanya tafiti za kina kwa manufaa ya Taifa.

Post a Comment

0 Comments