Na, CALVIN E. GWABARA
Wanafunzi wa wanne wa Mwaka wa tatu kutoka chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA wanaofanya tafiti shirikishi kwa kushirikiana na wakulima katika kupata ufumbuzi wa matatizo ya wakulima wa Mahindi Mkoani Morogoro kwa kutumia mbinu za asili kwa ufadhili wa Shirika la Kilimo Endelevu SAT wako mbioni kupata ufumbuzi wa tatizo la Viwavi jeshi vamizi.
Mwanafunzi Gloria Francis ( Mwenye Koti la Blue) akifafanua jambo kwa wakulima kuhusu utafiti wake wa kina cha shimo linalofaa kupanda mahindi.
|
Wakiongea na Waandishi wa habari katika eneo wanalofanyia utafiti kwenye shamba la SUA mmoja wa wanafunzi hao Matha Makumba anayefanya utafiti wa kutumia Unga wa majani ya Mlonge,Unga wa mbegu za Muarobaini na mchanganyiko wa mlonge na Muarobaini amesema kuwa matokeo ya awali yanaonesha Muarobaini umefanya vizuri.
Mwanafunzi huyo mtafiti amesema pamoja na kwamba muarobaini umefanya vizuri lakini bado kuna mashambulizi ya wadudu hao pamoja na kupuliza dawa hiyo kila baada ya wiki moja hivyo utafiti zaidi unatakiwa kufanyika kuweza kujua ni kwa namna gani maji ya mmea huo yanaweza kuboreshwa ili kupambana na wadudu hao.
Newton Kilasi Mhadhiri SUA na msimamizi wa wanafunzi hao (Kulia) akifafanua jambo. |
Pamoja na swala wa matumizi ya mbinu hizo za asili lakini pia walipanda mbegu tofauti tatu kuweza kubaini ni mbegu gani inayoweza kustahimili au kutoshambuliwa na wadudu hao ambapo walipanda mbegu aina za Staha,Meru na Tumbili lakini mbegu ya Tumbili imeonekana kutoshambuliwa zaidi na wadudu hao ikilinganishwa na mbegu hizo nyingine.
Kwa upande wake Glory Francis mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika ndaki ya Kilimo SUA ambaye amefanya utafiti kuona kina gani cha shimo kinatakiwa kupandwa mbegu ya mahindi ili iweze kuota vizuri baada ya wakulima kulalamika kuwa mbegu wanazopanda hazioti huku kukiwa na utofauti wa uchimbaji wa mashimo amesema kuwa yeye amebaini kuwa shimo la urefu wa sentimita tano ndilo linalofaa kupandwa mbegu.
Bi. Matha Makumba Mwanafunzi Mtafiti kutoka SUA anayefanya utafiti wa mbinu za asili za kukabiliana na Viwavijeshivamizi. |
Aidha amesema yeye alipanda kwenye mashimo ya urefu wa setimeta 15. 5 na sentimita 3 ili kuweza kujibu changamoto hiyo ya wakulima kutokana na wakulima hao kuwa na uchimbaji tofauti wa mashimo wengine yakiwa marefu na mengine mafupi lakini katika utafiti huo amebaini kuwa mbegu kubwa zimefanya vizuri kwenye sentimita 5.
Hata hivyo ameshauri wakulima kutumia mbegu kubwa kama ni msimu mzuri wa mvua kwani zinaweza kuota vizuri na kukua huku akishauri wakulima kuachana na kurudia mbegu za msimu uliopita na badala yake kila mwaka waende dukani kununua mbegu kwani kurudia mbegu kunapoteza sifa za mmea na kushusha uzalishaji.
Mtaalamu kutoka SAT BI: Elizabeth Dirangay akizungumzia umuhimu wa utafiti huo kwa wakulima hao na wanafunzi wanaofadhiliwa na Shirika lao la SAT.
|
Kwa upande wake mtafiti Neema Erasto ambaye anafanya utafiti wa kujua kwanini kunakuwa na uotaji hafifu wa mbegu amesema walitumia mbegu za asili na mbegu za dukani lakini pia kwa kutumia mbinu mbadala kwa kuloweka mbegu kwenye chumvi na kuloweka kwenye maji yasiyo na chumvi.
Amesema utafiti wake umebaini kuwa mbegu zilizolowekwa kwenye maji yasiyo na chumvi zimeota vizuri kuliko zile ambazo zililowekwa kwenye maji ya chumvi na zile ambazo hazikulowekwa kwakuwa zilizibeba unyevunyevu wa kutosha na zilipofika ardhini zimeota kirahisi zaidi na haraka.
Amesema zile zilizolowekwa kwenye chumvi zimeota kidogo kwakuwa zinapofika ardhini kunakuwa na ukizani wa kuvuta maji na hivyo kusababisha mbegu kuchelewa kuota na hivyo kuwashauri wakulima kutoloweka mbegu kwenye maji ya chumvi kama wanavyofanya na waloweke kwenye maji siku moja kabla ya kuzipanda ili zileinike na kuota haraka.
Akizungumzia utafiti huo wa wanafunzi hao Mtaalamu kutoka shirika la Kilimo endelevu SAT Bi. Elizabeth Dilrangay amesema shirika lao lina utaratibu wa kufanya tafiti shirikishi kwa kushirkiana na watafiti wa SUA kwa kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayoletwa na wakulima.
Amesema awamu ya kwanza waliwakutanisha wakulima na wafunzi na kisha wakulima wakaeleza changamoto zao ambapo wanafunzi hao wa SUA walipata maeneo ya kufanyia utafiti na kisha SAT kuwawezesha kutafuta ufumbuzi kwa kushirikiana nao kuanzisha mwanzo hadi mwisho na sasa wanawaleta wakulima kuona maendeleo.
Baada ya matokeo hayo kukamilika mwaka huu wataitisha mkutano mkubwa kwa kuwakutanisha pamoja wakulima,maafisa ugani na viongozi wa vijiji ili waweze kusikia na kujadiliana kwa pamoja namna nzuri za kutumia matokeo hayo yatakayotolewa na wanafunzi hao ili kuboresha kilimo chao.
Akizungumzia utafiti huo mmoja wa wakulima washirki wa utafiti bwana Manase Thomas kutoka kijiji cha kimambira ambaye ni mkulima wa kilimo hai amesema wamefurahia utafiti huo kwani unakwenda kujibu changamoto walizoziwasilisha kwa SAT na hivyo kutasaidia kuboresha kilimo chao.
Amesema mbuni zote zilizotumiwa na watafiti hao zimeleta matokeo chanya hasa katika matumizi ya mbuzu za muarobaini katika kuua viwavijeshi vamizi huku akiwataka wakulima wenzake wanaopenda kutumia mbegu walizovuna msimu uliopita sasa kuchagua mbegu nene na sio zile ndogondogo maana zinakuwa dhaifu.
0 Comments