SUAMEDIA

Mpango kabambe wa mifugo wa Mwaka 2017/2018 hadi 2021/2022 ni tumaini jipya kwa wafugaji nchini

Na Calvin Gwabara


Wadau wa Sekta ya Mifugo nchini wametakiwa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mpango kabambe wa mifugo wa Mwaka 2017/2018 hadi 2021/2022 ili kuwezesha kupunguza uhaba wa nyama na kuboresha maisha ya wafugaji nchini.

Mtaalam kutoka Dawati la Sekta binafsi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen Michael akijibu maswali kutoka kwa Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali wakati wa semina jijini Dodoma.


Wito huo umetolewa na Mtaalam kutoka Dawati la sekta binafsi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen Michael  wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano wa siku mbili ulioandaliwa na Jukwaa huru la wadau wa kilimo (ANSAF) kwa lengo la kuwajengea uwezo wanahabari kuripoti na kuishawishi Jamii na Serikali kuwekeza kwenye Sekta ya Mifugo na Uvuvi kuboresha sera inazosimamia.


Mtaalamu huyo amesema Tanzania imekuwa nchi ya pili kuanzisha mlango huo barani Afrika baada ya Ethiopia na hii ni baada ya kuona  Sekta ya Mifugo haijapewa kipaumbele kwenye mipango ya nchi hususani katika sera husika.
Waandishi wa Habari za mifugo nchini wakifuatilia mada zinazowasilishwa kwenye semina ya lengo la kuwajengea uwezo wanahabari katika kuripoti na kuishawishi Jamii pamoja na Serikali kuwekeza kwenye Sekta ya Mifugo na Uvuvi.
Amesema katika mpango huo waliangalia idadi ya mifugo na Mazao yake na wakaenda mbali zaidi kuangalia  kama idadi ya kila aina ya mfugo unatoa matokeo stahiki kulingana na Mazao tarajiwa.


Mtaalamu huyo kutoka Wizara ya mifugo na uvuvi ameongeza kuwa Mwaka  2016, Sekta ya mifugo na Uvuvi ilichangia asilimia 7.7 ya pato la taifa na ilikuwa kwa asilimia 2.6 huku kaya milioni 4.6 zilionekana kujishughulisha na mifugo.


Aidha ameongeza kuwa  Nyama nyekundu na nyeupe zinachangia kwa asilimia 40% kwenye pato la taifa, Maziwa asilimia 30% huku aina nyingine za Mazao ya mifugo zikichangia asilimia 30.


Amesema kuwa matokeo ya utafiti huo walioufanya wamegundua kuwa mahitaji ya nyama ni makubwa kuliko uzalishaji, vilevile kwenye maziwa lakini changamoto kubwa ni Magonjwa, malisho, maji pamoja na Mbari (Breed).
Washiriki na Viongozi wa ANSAF wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Mipango wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (mwenye miwani mstari wa mbele) Bw.Amos Zephania 
Bwana Michael amesema kufikia mwaka 2032 upungufu wa nyama nyekundu utakuwa tani 1,731,000 Sawa na asilimia 33 ya mahitaji huku eneo lililotengwa kwenye ufugaji ni asilimia 9.4 ya eneo la Taifa.

Ametoa wito kwa waandishi wa habari kujikita katika kutangaza Sekta ya Uvuvi na Mifugo pamoja  fursa zilizopo ili jamii iongeze kasi ya kushiriki na kutumia mazao yake yanayozalishwa kikamilifu





 kutoka kwenye sekta hiyo .

Post a Comment

0 Comments