Watahiniwa 91,442 wanatarajiwa kufanya mitihani yao ya kumaliza kidato cha sita kuanzia kesho Jumatatu Mei 6 hadi 23, 2019.
Mbali na hao, watahiniwa 12,540 wanatarajiwa kufanya mitihani yao ya kumaliza kozi ya ualimu katika ngazi ya cheti na stashahada.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Mei 5, 2019 Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde, amesema kumekuwa na ongezeko la watahiniwa wa shule wanaomaliza mtihani wa kidato cha sita kwa asilimia 4 ikilinganishwa na mwaka jana huku idadi ya watahiniwa wa ngazi ya ualimu wakiongezeka kwa asilimia 41.
Akitoa ufafanuzi wa watahiniwa wa mtihani wa kidato cha sita waliosajiliwa mwaka huu, amesema kati 80,305 ni watahiniwa wa shule na 11,117 ni wa kujitegemea
“Katika watahiniwa wa shule kati yao 46,224 sawa na asilimia 57.56 ni wavulana na 34,081 sawa na asilimia 42.44 ni wasichana huku watahiniwa walio na uhitaji maalumu wapo 102 kati yao, 67 ni wenye uoni hafifu; 16 ni wasioona; 18 wenye ulemavu wa kusikia; na 1 ni mwenye ulemavu wa afya ya akili,” amesema Dk Msonde.
0 Comments