SUAMEDIA

WAKULIMA WAILILIA SERIKALI KURUHUSU GMO


Na: Farida Mkongwe
Mahindi ni moja ya zao la nafaka linaloongoza kulimwa na wakulima wengi hapa nchini na barani Afrika kwa ujumla. Kwa kiasi kikubwa mahindi hulimwa kama zao la chakula, lakini likilimwa vizuri linaweza kutumika kama zao la biashara iwapo mavuno yake yatakuwa mengi na mazuri.
Wakulima wa zao hili la mahindi ambalo kwa Tanzania ndiyo zao kuu la chakula wamekuwa  wakikabiliwa na changamoto mbalimbali yakiwemo mabadiliko ya tabianchi ambayo  yamesababisha ukame wa mara kwa mara , ukosefu wa mbegu bora za mazao na mifugo, visumbufu na magonjwa ya mimea na mifugo pamoja na Matumizi  ya teknolojia duni ambavyo kwa pamoja vimemsababishia mkulima kuwa na uzalishaji duni wa mazao.
Kiwavi jeshi vamizi ajulikanae kama Fall Armyworm au kwa jina la kitaalamu “Spodoptera frugipedra” asili yake ikiwa ni bara la America ni mdudu ambaye ameacha kilio kikubwa kwa wakulima hasa katika msimu wa mwaka huu wa kilimo. Baadhi ya wakulima ambao mashamba yao yamevamiwa na viwavi jeshi vamizi wamesema hasara kubwa waliyoipata mwaka huu imewafanya wafikie hatua ya kukata tamaa ya kuendelea na shughuli za kilimo.
viwavi
Kiwavi jeshi vamizi akishambulia mahindi
Hata hivyo hatua kadhaa zilichukuliwa ili kukabiliana na mdudu huyo hatari anayeleta tishio la njaa hapa nchini, hatua mojawapo yenye kuonesha uhai na mafanikio kwa wakulima ni ile ya utafiti wa teknolojia ya uhandisi jeni GMO.
Utafiti wa uhandisi jeni katika maabara unafanyika katika Kituo cha Utafiti cha Kilimo kilichopo Mikocheni jijini Dar Es Salaam huku utafiti wa nje ya maabara ukifanyika katika shamba maalumu lililopo katika kituo cha Utafiti cha Makutupora jijini Dodoma ambapo utafiti unaofanyika hapo ni kwa ajili ya utafiti wa mahindi yanayovumilia ukame na yenye ukinzani dhidi ya mdudu bungua.
MATOKEO YA AWALI YA UTAFITI HUO
Tathmini ya Matokeo ya awali ya utafiti wa mbegu iliyowekwa vinasaba (GMO) unaofanyika kwenye  Kituo cha Utafiti wa Kilimo Makutupora jijini Dodoma umeonesha kuwa mahindi ya GMO yameweza kustahimili mashambulizi ya bungua na viwavi jeshi vamizi kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na mbegu nyingine.
Mtafiti na Mgunduzi wa Mbegu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania TARI kituo cha Ilonga Dkt. Justin Ringo amethibitisha hilo wakati akitoa ufafanuzi kwa wakulima na waandishi wa habari  waliotembelea  kwenye kituo hicho kwa lengo la kujionea tofauti iliyopo kati ya mbegu za GMO na mbegu chotara ambazo zimekuwa zikitumiwa na wakulima wengi hapa nchini.
“Utafiti huu utakapokamilika na kuruhusiwa kutumika kwa mbegu hizi za GMO nchini kutasaidia kuongeza mafaniko kwa wakulima kwani mbegu hizi zina faida nyingi kutokana na uwezo wake wa kuhimili mdudu aina ya kiwavi jeshi vamizi na kustahimili ukame”, alisema Dkt. Ringo.
Alizitaja faida nyingine za kutumia mbegu za GMO kuwa ni kuongezeka kwa mavuno ya mahindi kwa wastani wa asilimia 35 katika maeneo yenye upungufu wa mvua, kuongezeka kwa uzalishaji wa mahindi kutoka takribani tani milioni 7-8 kwa mwaka hadi tani milioni 15-18 kutokana na kupungua kwa mashambulizi ya bungua wa mahindi.
Faida nyingine ni pamoja na ongezeko la usalama wa chakula na lishe kwa ngazi ya kaya na taifa kwa jumla na kupungua kwa matumizi ya viuatilifu vya kumdhibiti bungua wa mahindi kwa kiasi cha asilimia 100 na hivyo kupungua kwa gharama za uzalishaji na kuchangia katika kuboresha afya za wakulima wa mahindi na katika kuhifadhi mazingira.
vviwav
Baadhi ya waandishi wa habari wakifanya mahojiano na Mgunduzi wa mbegu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania Kituo cha Ilonga Dkt. Justin Ringo.
WAKULIMA WALIOTEMBELEA KITUO CHA UTAFITI MAKUTUPORA WANASEMAJE?
Wakulima waliotembelea  Kituo cha Utafiti cha Makutopora jijini Dodoma wameiomba serikali kuharakisha mchakato wa matumizi ya teknolojia ya uhandisi jeni GMO pindi watafiti watakapokamilisha taratibu za kiutafiti kwa kuwa teknojolojia hiyo imeonekana kuwa mkombozi wa mkulima.
Wakulima hao Ivan Mwalimu , Petro Matigu, Valentina Ally na Mohamed Rajabu kutoka vijiji tofauti vilivyopo kata ya Makutupora walisema mahindi hayo ya GMO  ni yenye ubora kutokana na kutoshambuliwa na wadudu na kustahamili ukame.
“Mwaka huu wakulima wengi wa mahindi tumepata hasara kubwa kutokana na wadudu aina ya viwavi jeshi vamizi kushambulia mazao yetu na kutufanya tukate tamaa kabisa kuendelea na kilimo lakini kwa hali tuliyoiona hapa jinsi mahindi haya ya GMO yalivyostawi tunaiomba serikali ifanye kila namna ili ituletee mbegu hizi, tuna imani zitatukomboa”, walisema wakulima hao kwa nyakati tofauti.

MSIMAMO WA TUME YA SAYANSI NA TEKNOLOJIA (COSTECH) KUHUSU UTAFITI WA GMO
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH)  Dkt. Amos Nungu alisema tume hiyo ina jukumu kubwa la kufanikisha utafiti huo wa mbegu za GMO ambao unalenga kutatua changamoto kubwa zinazowakabili wakulima nchini.
“Kama tume ni jukumu letu kufanikisha utafiti wa teknolojia hii na tunawaruhusu wadau wengine waje kujionea ukweli wa mambo ulivyo ili kuondoa mashaka ambayo wanaweza kuwa nayo”, alisema Dkt.Nungu.
Alibainisha kuwa utafiti huo ni wa pili na wa mwisho kufanyika katika kituo hicho baada ya kukamilika wataishauri serikali kuhusu matumizi ya teknolojia hiyo na iwapo serikali itaridhia kutokana na matokeo yatakayojitokeza basi changamoto hizo kubwa za wakulima zitakuwa zimepata majibu.
Utafiti huo wa Teknolojia ya Uhandisi Jeni unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu baada ya mahindi hayo kuvunwa.
picha ya mahindi
Upande wa kushoto mahindi yenye kibao GM ENT.7 ni mahindi yaliyopandwa kwa kutumia mbegu za GMO, upande wa katikati kwenye kibao  NON GM ENT.8 ni mbegu chotara zinazotumiwa na wakulima

Post a Comment

0 Comments