SUAMEDIA

Nufaika kwa kilimo bora cha binzari


Jina la kitalaam ni Curcuma domestica au Curcuma longa na kwa kiingereza niturmeric.

Zao hili asili yake ni Mashariki ya Mbali, na linalimwa zaidi katika mkoa wa Tanga,
Kagera, Kilimanjaro, Morogoro na Zanzibar. Binzari hutumika kwa mapishi ya nyama,
samaki na mapishi mengine kwa kuweka rangi yake ya njano. Hutumika zaidi na nchi
za mashariki kama India; nchi za Ulaya hutumia kidogo sana.

Mahitaji na mambo muhimu katika uzalishaji;

Hali ya hewa
Humea vizuri maeneo yenye kiasi cha joto la nyuzi 24-26 za sentigredi na huzalishwa
maeneo ya mwambao.

Udongo
Udongo wenye rutuba na unaopitisha maji na usio na mawe au changarawe. Mahitaji ya
mvua ni milimita 1200-2000 kwa mwaka. Epuka kusimama kwa maji shambani.

Umwagiliaji unaweza kufanywa endapo maji hayatoshelezi. Binzari inafanya vizuri
ikipandwa sehemu ya uwazi. Ingawa pia inaweza kuchanganywa na mazao mengine
kama minazi.

Uchaguzi wa mbegu
Mbegu zinazotumika hapa nchini ni za kienyeji bado. Tunguu kubwa zenye ukubwa wa
sm 2.5 hadi sm 3 hutumika kama mbegu. Kiasi cha tani 1.7 za vipando huhitajika kwa
hekta. Tunguu za kupandwa zisihifadhiwe kwa zaidi ya mwezi mmoja kabla ya
kupanda.

Nafasi ya upandaji
Nafasi ya kupanda ni sm 15-25 kati ya mmea na mmea na sm 25-30 kati ya mstari na
mstari au sm 45-60 kati ya tuta na tuta.

Mahitaji ya mbolea
Matumizi ya mbolea hapa Tanzania si makubwa katika kilimo cha viungo. Tafiti
zimeonesha kuwa binzari hazioneshi kufanya vizuri kwenye mbolea za viwandani.
Mbolea za samadi zinaweza kutumika. Kiasi cha tani mbili hadi tatu za samadi kwa eka
moja kinatosha.

Uvunaji
Uvunaji hufanywa kwa kutumia majembe au uma. Binzari huvunwa wakati majani
yamegeuka rangi na kuwa njano au kahawia. Binzari isiyo na kambamba huvunwa
kipindi cha miezi sita toka kupandwa na miezi 18 hadi 21 kwa binzari iliyokomaa
kutegemeana na mahitaji ya soko.

Mavuno ya tani 7 hupatikana endapo binzari ikipandwa peke yake. Mavuno hupungua
kiasi binzari ikipandwa mchanganyiko na mazao mengine kwa mfano mavuno ya tani
4.8 kwa hekta yatapatikana binzari ikipandwa na minazi.

Utayarishaji
Kabla ya kuhifadhiwa binzari zichemshwe kwa dakika 45 hadi saa moja ili kuondoa
harufu yake ya udongo. Pia kuchemsha kunasaidia zikauke kwa pamoja. Binzari
zichemshwe  mpaka kijiti kisicho na ncha kali kiweze kutoboka kwa urahisi. Kisha
ziepuliwe na  kuanikwa juani kawaida huchukua siku 10 hadi 15 ili zikauke kufikia kiasi
cha unyevu (moisture content) 5% hadi 10%. Binzari pia yaweza katwa vipande vidogo
vidogo ili kurahisisha kukauka. Baada ya hapo ziko tayari kutwangwa au kusagwa
kwenye mashine za kusagia viungo au kuhifadhiwa kama zilivyo.

Mashambulizi ya wadudu na magonjwa
Tatizo kubwa ni ugonjwa wa ukungu unaosababishwa na vimelea vinavyoitwa
Colletotrichum sp.na Glomerella cingulata. Dalili ni madoa ya kahawia kwenye majani
ambayo husambaa na kisha jani hukauka. Magonjwa haya yanaweza kudhibitiwa kwa
kupiga dawa za ukungu kama Dithane M-45 kila baada ya wiki mbili.

Masoko
Soko la binzari linapatikana ndani na nje ya nchi.. Zao hili huuzwa katika nchi za
Uganda, Kenya, Uingereza, Ujerumani, Mashariki ya Kati, n.k. Binzari yaweza kuuzwa
ikiwa mbichi (mara tu baada ya kuvuna), ikiwa kavu au baada ya kusagwa kulingana na
mahitaji ya soko.

Ushauri: Wakulima wanashauriwa kukausha binzari kwa uangalifu ili kutoharibu ubora wake.

Post a Comment

0 Comments