SUAMEDIA

Waziri Mhagama Awaonya Waajiri Wote Kutonyanyasa Wanawake

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe.Jenista mhagama amewataka waajiri wote nchini kutonyanyasa wanawake katika masuala ya kazi ili kuwa na usawa maeneo ya kazi.

Ameitoa kauli hiyo hii jana tarehe 30 Aprili, 2019 alipokuwa akifungua semina ya siku moja ya viongozi wanawake kutoka vyama mbalimbali vya wafanyakazi nchini walipokutana kujadili masuala yanayowahusu wawapo kazini ikiwemo; haki na wajibu wao wawapo kazini iliyofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Paradise Inn Jijini Mbeya.




Waziri alieleza kuwa waajiri hawana budi kubadili mitazamo hasi iliyopo katika jamii ya kuona wanawake ni viumbe dhaifu na wenye majukumu mengi yanayoweza kukwamishi jitihada zao wawapo kazini badala yake wawaone kuwa ni viungo muhimu katika kuchangia uzalishaji na maendeleo nchini.

“Mchango wa wanawake ni mkubwa endapo utatambuliwa na kuthamini katika nyanja zote za ukuaji wa uchumi, hivyo ni vyema maeneo ya kazi waajiri watimize wajibu wao kwa kundi hili kwa kuzinigatia sheria zilizopo na wasinyanyaswe na waendelee kuheshimiwa na kupewa haki na stahiki zao kama wafanyakazi wengine.”alisisitiza Waziri Mhagama.

Waziri alieleza jitihada za serikali ni kuhakikisha inasimamia vyema sheria na taratibu za kazi nchini kwa kuliangalia kundi hili ili kuwa na waajiriwa wenye kuzingatia usawa wa kijinsia.


“Ninakemea vitendo vya unyanyasaji wa haki za wanawake kazini ikiwemo kukoseshwa haki zao na vyama hivi vya wafanyakazi viendelee kuleta tija katika kukemea matendo hayo,”alisistiza Waziri Mhagama.

Aidha Waziri aliwataka wanawake kuendelea kuvitumia vyama vya wafanyakazi kama jukwaa maalum la kueleza na kutatua changamoto zao.

Aliongezea kuwa, pamoja na changamoto wanazokutana nazo wanawake hawana budi kujiendeleza kielimu ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yaliyopo katika masuala ya kazi.

“Wanawake umefika wakati kuendelea kujiendeleza katika eneo la elimu ili kuwa na vigezo mahususi vitakavyo wapa nafasi nzuri katika maeneo yenu ya kazi.”alisisema Waziri Mhagma.

Naye rais wa Shirikizo la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Bw. Tumaini Nyamhokya alimpongeza waziri pamoja na changamoto zilizopo katika kufikia haki sawa kwa wote , alieelza umuhimu wa kuendelea kuliinua kundi hili ili kuwasaidia wanawake wa Kitanzania katika kupata haki na usawa kwenye maeneo yao ya kazi.

“Wanawake wana uwezo mkubwa hivyo tuendelee kujali na kutunza nafasi zao wawapo kazini ili kuwezesha Taifa kuendelea kuwa na maendeleleo,” alisisitiza Nyamhokya.

Kwa upande wake Mwenyekiti Kamati ya Wanawake Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Bi. Rehema Ludanga alieleza kuwa, ni wakati sahihi kuendelea kuchangamkia fursa za maendeleo ikiwemo uanzishwaji wa viwanda vya wanawake vitakavyosaidia kuondokana na hali ya utegemezi na kuchangia katika ongezeko la uzalishaji nchini.

Post a Comment

0 Comments