Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kimetakiwa kufahamu kuwa kina dhamana kubwa ya kumuenzi kwa vitendo Hayati Edward Moringe Sokoine kutokana na kubeba jina lake, hivyo wana kila sababu ya kuyafanya yale yote aliyokuwa anayafanya wakati wa uhai wake katika Sekta ya Kilimo.
Akifunga Kumbukizi ya Hayati Edward Moringe Sokoine Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amekitaka Chuo cha SUA kutambua kuwa wana dhamana ya kuhakikisha wanatambua hilo na hasa katika kuleta mapinduzi ya Sekta ya Kilimo hasa kwa kuyaishi na kuyaenzi.
Kwa upande mwingine amesema Serikali katika kutambua umuhimu wa Sekta ya kilimo imeendelea kukiwezesha Chuo Kikuu Cha Sokoine cha Kilimo SUA ikiwemo kuwezesha katika ujenzi wa Maabara Mtambuka, pamoja na Maabara ya Udongo ikiwemo Mabweni na Karakana za Uhandisi Kilimo.
Aidha amefafanua kuwa “Serikali ya awamu ya tano kupitia Wizara ya Elimu imeendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia ili kuweza kuzalisha wataalamu watakao leta mageuzi katika Sekta ya Kilimo”. Amesema waziri Ndalichako.
Akijibu hoja ya mwanafunzi wa shule ya Sekondari Mafiga Bw. Kishosha Musa iliyopo mjini Morogoro aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wakuzirudisha shule za kilimo ili Kilimo kiweze kujengewa msingi toka chini, Waziri Ndalichako ameahidi kufufua shule za ufundi zinaanza kazi na kuhakikisha ifikapo Januari mwakani shule hizo zinaanza kufundisha lakini pia suala la shule za kilimo kuhakikisha analifanyia kazi kwa vile yeye anadhamana yaWizara ya Elimu nchini.
Mwanafunzi huyo akichangia katika mdahalo huo ameeleza kuwa kurudishwa kwa shule za Kilimo zitasaidia kuongeza ari kwa wanafunzi kujikita katika masuala ya Kilimo na hivyo azma ya Serikali ya kufikia Uchumiwa wa Viwanda inafikiwa.
Awali kabla ya kufungwa kwa wiki ya kumbukizi ya Hayati Edward Moringe Sokoine kulitanguliwa na Mdahalo wa Kitaifa ambapo Mwanasiasa mkongwe, Mh. Getrude Mongela ambaye alikuwa mchokoza Mada kuhusu NAMNA ALIVYO MFAHAMU SOKOINE NA MCHANGO WAKE KATIKA KILIMO, amesema hayati Edward Moringe Sokoine wakati wa uhai wake alipambana vikali na vitendo vya uhujumu uchumi na kuhimiza kila mtu kufanya kazi.
Mama Mongela amemuelezea Sokoine kuwa alipenda kuuliza “Nifanye nini ili niweze kuwatoa wakulima katika Jembe la Mkono? ”, lakini pia Sokoine katika uhai wake alikuwa mtu anayejiamini na wakati wote alikuwa akipenda kufanya kazi na kutoa maelekezo ya kiutendaji kwa viongozi na wananchi.
Ameongeza kuwa Sokoine aliamini kila wakati ni muda wa kazi na alifanya kazi kwa saa 24 kwani alikuwa ni mtu wa kujituma lakini pia alijali sheria na utaratibu, pia alikuwa mnyenyekevu na mwenye upendo kwa watu, pamoja na kuimarisha dhana na misingi ya Utawala Bora.
Kwa upande wake Prof. Amon Matee kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA ambaye alijikita katika mada inayozungumzia MCHANGO WA KILIMO KATIKA MAENDELEO YA VIWANDA amesema ili kuweza kuwa na maendeleo ya Viwanda ni muhimu kuwaboreshea Wakulima Mazingira yao katika shughuli zao kwani wao ni sehemu kubwa ya Soko la malighafi zinazohitajika Viwandani.
Amefafanua kuwa ni muhimu kuwajengea uwezo Wakulima ili waweze kuzalisha kwa wingi na kwa ubora kwani kunapokuwa na mahitaji makubwa ya kitu chochote kunahitajika pia kuwe na uzalishaji mkubwa nawa kutosheleza.
0 Comments