SUAMEDIA

MKUTANO WA MENEJIMENTI YA CHUO NA MENEJIMENTI YA BENKI YA CRDB



Benki ya CRDB imetangaza bidhaa yao mpya iitwayo “Salary Advance” kwa Watumishi wa umma ambapo ilifanya mkutano wake na Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo siku ya Jumatatu tarehe 09/10/2017.
Mwenyekiti wa Mkutano huo Prof. Y.M. Ngaga, Naibu Makamu wa Mkuu wa Chuo (Utawala na Fedha ) alifungua mkutano huo kwa kumtambulisha Kiongozi wa msafara wa Menejimenti ya Benki  Bi. Grace Maseki, Meneja wa Benki ya CRDB tawi la SUA ambaye aliongozana na Viongozi mbalimbali kutoka Makao makuu ya Benki ya CRDB.

Bidhaa hiyo ya “Salary Advance” inatolewa kwa wafanyakazi wa serikali ambao mishahara yao inapitishiwa katika akaunti za benki ya CRDB ambapo riba ya mkopo huu ni asilimia 5 tu ya mkopo unaokopwa na riba hiyo inakatwa kabla ya mkopo kutolewa hivyo mshahara unapotoka kiasi unachokatwa ni kiwango cha mkopo tu uliokopa.

Imeelezwa na maafisa hao kutoka CRDB kuwa,  vigezo vya kumfanya mtumishi huyo wa serikali kupata mkopo huo ni kwa mfanyakazi ambaye mshahara wake unapitia benki ya CRDB ili utakapokopa iwe rahisi kurejesha deni wakati mshahara unapoingia, uwe umejiunga na huduma ya “CRDB Simbanking” ambayo ndio njia rahisi ya kuupata mkopo wako na kuweza kulipa deni la mkopo wako.

Aidha Meneja Mikopo ya Biashara wa CRDB, Bi. Theo Madilu alisisitiza kwamba  bidhaa hii ya “Salary Advance” haina makato makubwa ukilinganisha na watoaji mikopo wengine ambao wanafikia hata riba ya asilimia 50 na hivyo kumweka mkopaji katika wakati mgumu anaporejesha mkopo wake.

Inapotokea mkopaji kachelewa kurejesha mkopo wake baada ya siku thelathini na tano za ahueni atatozwa faini ya asilimia 0.3 kwa kila siku inayozidi hapo hadi atakaporejesha mkopo wake.

Aidha imesisitizwa kuwa kwa mfanyakazi ambaye ana mkopo wa fao jingine ndani ya CRDB mkopo huo haumzuii kukopa “ Salary Advance”  kwa vile mkopo huu unahusika na fedha taslimu ya mshahara tu. Hata inapotokea katika akaunti ya mteja kuna fedha nyingine yoyote mkopo huu hautakata fedha hiyo isipokuwa unasubiri fedha ya mshahara iingine ndipo wanapokata deni lao.

Ilisisitiza pia kuwa mkopo huu ni vizuri kuufanya kama wa dharura na sio wa kukopa mara kwa mara ili kuepuka usumbufu kwa mfanyakazi kibajeti ambapo kima cha chini cha kukopa ni shs 50,000/= na kima cha juu cha kukopa ni asilimia 50 ya fedha taslimu anayopokea mfanyakazi kama mshahara wake.

B. I. Kadago
Kaimu Afisa Mawasiliano na Masoko
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo.

Post a Comment

0 Comments