SUAMEDIA

SUA yaboresha mitaala yake kuzalisha wahitimu watakaotoa ajira kwa wengine.

NA; Ayoub Mwigune - Morogoro. 

Katika kuondokana na changamoto ya ajira Chuo cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kipo katika hatua ya Kuandaa na Kuboresha Mitaala ya Elimu ili kuweza kupata Wataalam, kutengeneza Wanafunzi ambao baadae wataweza kutengeneza ajira na watakaoleta bidhaa na huduma mpya nchini.

Mkurugenzi wa Shahada za Awali Dkt. Nyambilila Amuri wa kwanza kushoto akimkabidhi zawadi cheti na fedha taslimu shilingi milioni moja na nusu kwa mwanafunzi fikiri matatizo mwenye fulana nyeupe aliyeibuka mshindi katika kuwasilisha bunifu kwenye kongamano.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Shahada za Awali Dkt. Nyambilila Amuri wakati akimuwakilisha Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam Prof. Esron Karimuribo wakati wa kuhitimisha Kongamano la Wadau wa Viwanda na Taasisi za Elimu ya Juu lililoambatana na utoaji tuzo na zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika kuwasilisha bunifu zenye tija

Aidha Dkt. Nyambilila amesema kupitia kongamano hilo sambamba na ushiriki wa vijana katika kuwasilisha bunifu zao kunathibitisha namna ambavyo Chuo hicho kimepiga hatua katika na kuweza kupata wataalam, kuwaandaa wanafunzi ambao baadae wataweza kutengeneza ajira na watakaoleta bidhaa na huduma mpya nchini.

“Katika kutekeleza haya tunakwenda kufanya mapitio ya mitaala na kuboresha mitaala itakayowezesha wanafunzi kupata ujuzi zaidi sisi ni wataalumu wa kisasa tunasikiliza wanafunzi kama tulivyowasikiliza leo , mwanafunzi mwenye changamoto , wazo lolote au bunifu yoyote aje hii ni namna ya kuweza kuwasaidia wanafunzi ”, amesema Dkt. Nyambilila

Akielezea kuhusu Sekta binafsi amesema kwa sasa milango ipo wazo kwa Chuo kuendelea kushirikiana kwa kufuata taratibu ili kuweza kuchukua hatua katika utekelezaji wa ushirikiano kati ya Taasisi binafsi , Viwanda pamoja na Vyuo ili kuweza kufikia malengo yatakayoweza kusaidia kuondoa changamoto mbalimbali.

kwa Upande wake Dkt. Felix Nandonde ambaye ni Mhadhiri wa Chuo cha SUA na Mratibu wa Mradi wa HEET katika eneo linalounganisha Viwanda na Taasisi za Elimu ya Juu amewashukuru wadau mbalimbali ambao wameshiriki katika Kongamano hilo huku akisisitiza zaidi kuendelea kuwa na ushirikiano ili kuweza kufanikisha malengo mbalimbali.

Naye Makamu Mwenyekiti Chemba ya Viwanda na Biashara Prof Faustine Lekule amesema kupitia Kongamano hilo kunatoa somo kubwa kwa vijana wa SUA ambao wanatarajia kuingia kwenye soko la ajira hasa katika kuandika maandiko yenye mashiko katika jamii na kuweza kuwanufaisha kupata ajira katika sekta mbalimbali huku akishukuru Chuo kwa kuandaa Kongamano hilo.

Kongamano hilo liliambatana na utoaji wa vyeti na fedha taslimu kwa wanafunzi ambao walishinda katika kuwasilisha bunifu zao mbalimbali ambapo Mwanafunzi wa Shahada ya Kwanza ya Ualimu wa Fizikia na Tehama Fikiri Matatizo aliweza kukabidhiwa kiasi cha shilingi Milioni 1.5 pamoja na cheti huku mshindi wa pili akikabidhiwa zawadi ya shilingi Milioni moja pamoja na cheti wakati mshindi wa tatu akikabidhiwa shilingi 500,000 pamoja na cheti 

Akielezea baada ya kuondoka na ushindi Fikiri Matatizo amesema kupitia fedha ambazo amekabidhiwa zitaweza kumsaidia katika kuboresha bunifu yake ili iweze kufika mbali zaidi huku akitoa wito kwa wanafunzi wenzake kuendelea kufanya bunifu zenye tija katika kilimo ili waweze kujiajiri na kutatua changamoto mbalimbali zilipo katika sekta hiyo.


Wanafunzi mbalimbali kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA ambao wamefanikiwa kuwa washindi katika kuwasilisha bunifu zao katika kongamano la Wadau wa Viwanda na Taasisi za Elimu ya juu.

 


Washiriki katika Kongamano la Wadau wa Viwanda na Taasisi za Elimu ya Juu wakisikiliza jambo kwa umakini.



Post a Comment

0 Comments