Na: Ayoub Mwigune
Wajasiriamali, wakulima na wafugaji nchini wanatarajiwa
kunufaika zaidi na teknolojia, mafunzo na ubunifu unaotokana na tafiti za Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia ushirikiano wake na Taasisi ya
Kuwajengea Uwezo Wajasiriamali katika Harakati za Kujiletea Maendeleo (AICAD).
Ushirikiano huo unalenga kuongeza tija, thamani ya mazao na kipato cha
wananchi.
Hayo yameelezwa na Afisa Programu wa AICAD, Bw. Florence Rugimbana, alipokuwa akizungumza na SUA Media katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere wakati wa Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki yaliyofanyika mkoani Morogoro.
Bw. Rugimbana amesema AICAD hufanya kazi kwa kushirikiana na
SUA, vyuo vikuu na taasisi nyingine za utafiti ili kuwafikishia wajasiriamali,
wakulima na wafugaji teknolojia na bunifu zinazotokana na tafiti. Amefafanua
kuwa jukumu kuu la taasisi hiyo ni kuwa daraja kati ya wabunifu wa teknolojia
na watumiaji wake.
Amesema kupitia ushirikiano huo, AICAD hutoa mafunzo kuhusu matumizi ya teknolojia mbalimbali, hususan katika sekta ya kilimo, ili kuwawezesha wananchi kuongeza uzalishaji, thamani ya mazao na kipato chao.
Aidha, amesema taasisi hiyo hufanya tafiti katika jamii ili
kubaini changamoto na fursa zilizopo, kisha hushirikiana na taasisi za utafiti
kutafuta teknolojia na suluhisho zinazofaa kwa wakulima, wafugaji na
wajasiriamali.
“Tumekuja katika Maonesho haya ya Nanenane kwenye banda la SUA kuwafahamisha wananchi kuhusu AICAD na kuonesha baadhi ya bidhaa zinazozalishwa na wahitimu wa mafunzo yetu, ikiwemo bidhaa za mazao ya kilimo zilizoongezwa thamani pamoja na bidhaa zinazotokana na uboreshaji wa kazi za mikono,” amesema Bw. Rugimbana.
Ameongeza kuwa ushirikiano huo unatoa fursa kwa wananchi
kupata maarifa, teknolojia na ujuzi unaoweza kuwasaidia kuboresha shughuli zao
za uzalishaji, kuongeza ubora wa bidhaa na kupanua fursa za kiuchumi.
.JPG.jpeg)
.JPG.jpeg)
.JPG.jpeg)
0 Comments