Na: Farida Mkongwe
Hali ya usalama imeimarishwa katika mabanda ya Chuo Kikuu
cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwenye Maonesho ya Nanenane, huku Mrakibu wa
Polisi Msaidizi katika Idara ya Usalama, Nicholaus Mwantobe, akisema hatua
mbalimbali zimechukuliwa kuhakikisha watumishi, wageni na mali zao zinakuwa
salama wakati wote.
Mwantobe, ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Usalama SUA, amesema askari wanaendelea kufuatilia hali ya usalama katika maeneo yote ya maonesho, yakiwemo mabanda, maeneo ya maegesho ya vyombo vya usafiri pamoja na sehemu zinazotumiwa na watumishi na wananchi wanaotembelea maonesho hayo.
Amewataka watumishi na wageni kuendelea kuwa waangalifu na
mali zao binafsi, akieleza kuwa pamoja na uwepo wa askari, kila mtu ana wajibu
wa kuchukua tahadhari kwa kuwa askari hawezi kuwa karibu na kila mwananchi
wakati wote.
Aidha, ametoa onyo kwa mtu yeyote mwenye nia ya kufanya uhalifu katika eneo la maonesho, akisema vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga na vina askari wenye weledi wa kutosha.
Amewahakikishia watumishi na wananchi kuendelea na shughuli
zao bila hofu, huku akisisitiza kuwa hatua stahiki zitachukuliwa dhidi ya
yeyote atakayejaribu kufanya uhalifu.
0 Comments