SUAMEDIA

Mtanzania Rehema Katuga aibuka mshindi uchaguzi wa Baraza la CALC.

Na: Mwandishi wetu.

Mtanzania Bi. Rehema Katuga kutoka Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria nchini (OCPD) ameibuka mshindi katika uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Uongozi na Usimamizi la Chama cha wataalamu wa Uandishi wa sheria wa Jumuiya ya Madola (CALC), na kuwa mmoja wa wawakilishi wa Afrika katika baraza hilo.

Bi. Rehema Katuga ambaye ni Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Urekebu Utafiti na Mafunzo kutoka Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD)

Baraza hilo lenye wawakilishi wawili kutoka kila bara linasimamia na kufanya maamuzi muhimu kuhusu uendeshaji wa chama hicho cha kitaaluma cha wataalamu wa uandishi wa sheria katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola.

Bi. Katuga ameibuka mshindi katika uchaguzi uliowahusisha wagombea wanne kutoka Afrika, wakiwemo wagombea wawili kutoka Afrika Kusini, mmoja kutoka Namibia na yeye akiwa muwakilishi pekee kutoka Tanzania, hivyo kuiwezesha Tanzania kupata nafasi ya uwakilishi katika chombo hicho muhimu cha kitaaluma.

Akizungumza kuhusu umuhimu wa CALC, imeelezwa kuwa chama hicho ni miongoni mwa vyama vya kitaaluma vinavyosimamiwa na Jumuiya ya Madola na kina jukumu la kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wataalamu wa uandishi wa sheria katika nchi wanachama.

“CALC inalenga kuimarisha uwezo wa wataalamu hao katika kuandaa sheria bora zinazoweza kutafsiri sera za Serikali na kubeba mageuzi mbalimbali yanayohitajika katika nchi, huku ikisisitiza ushirikiano katika mafunzo, kubadilishana uzoefu, programu za mafunzo kwa vitendo (attachments), matumizi ya teknolojia katika uandishi wa sheria na kuendeleza mbinu bora za uandishi wa sheria” alieleza Bi Katuga.

Aliongeza “Lakini pia cham hiki kina Baraza la uongozi linalojumuisha viongozi wakuu pamoja na wawakilishi kutoka mabara mbalimbali ambao ndio sisi tuliochaguliwa sasa, ambao kwa pamoja hushiriki katika kutoa mwelekeo na kufanya maamuzi kuhusu maendeleo ya taaluma ya uandishi wa sheria”.

Muwakilishi huyo wa Tanzania na Afrika amesema kupitia nafasi hiyo aliyoipata itamuwezesha kuchangia kutoa fursa kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla kuimarisha ushirikiano wa wataalamu wa uandishi wa sheria, kubadilishana maarifa na uzoefu na nchi nyingine za Jumuiya ya Madola, pamoja na kujifunza na kutumia mbinu bora za kisasa katika uandishi wa sheria.

Aidha amesema anatarajiwa kushiriki kikamilifu katika kuunganisha wataalamu wa uandishi wa sheria barani Afrika, kukuza taaluma hiyo na kuchangia katika juhudi za kuboresha ubora wa sheria kupitia uandishi wenye weledi, uwazi na ufanisi.

Kwa Tanzania uwakilishi huo pia unaongeza nafasi ya nchi kushiriki katika majadiliano ya kimataifa kuhusu maendeleo ya taaluma ya uandishi wa sheria na kunufaika na fursa za mafunzo, kujengea uwezo wataalamu wa fani hiyo nchini na ubadilishanaji wa teknolojia na uzoefu, hatua inayoweza kusaidia kuimarisha ubora wa mchakato wa uandaaji wa sheria nchini.

Matokeo hayo ya Uchaguzi yalitangazwa kwenye mkutano Mkuu wa Chama hicho uliofanyika tarehe 19 mwezi huu nchini Singapore.

 

                                                     

Post a Comment

0 Comments