SUAMEDIA

Waziri Mkuu aweka jiwe la msingi jengo la taaluma na bweni SUA

 Na: Mwandishi wetu

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kinaendelea kuimarisha miundombinu ya elimu katika Kampasi ya Mizengo Pinda kupitia ujenzi wa jengo la taaluma na bweni la wanafunzi kwa ufadhili wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), hatua inayolenga kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

Akizungumza katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi iliyofanyika tarehe 14 Machi, 2026, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya elimu ya juu ili kuongeza ubora wa mafunzo, tafiti na huduma kwa jamii.

Aidha, Waziri Mkuu amewahimiza wanafunzi kutumia kikamilifu fursa ya maboresho ya miundombinu ya elimu yanayofanywa na Serikali kwa kusoma kwa bidii na kujenga msingi imara wa taaluma zao ili waweze kuchangia maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu, Prof. Maulid Mwatawala, akimwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Prof. Raphael Chibunda, amesema ujenzi wa jengo la taaluma na bweni katika Kampasi ya Mizengo Pinda utasaidia kuongeza uwezo wa chuo kupokea wanafunzi wengi zaidi, kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, pamoja na kuimarisha utoaji wa elimu bora.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, watumishi wa chuo pamoja na wanafunzi wa SUA waliokusanyika kushuhudia hatua hiyo muhimu ya maendeleo ya miundombinu ya elimu katika chuo hicho.

Ujenzi wa miundombinu hiyo unatarajiwa kuimarisha zaidi dhamira ya SUA ya kutoa elimu bora, kufanya tafiti zenye tija na kutoa huduma kwa jamii katika sekta za kilimo, mifugo, misitu na sayansi zinazohusiana na maendeleo ya taifa.





Post a Comment

0 Comments