Na: Ayoub Mwigune
Mkutano Mkuu wa nne wa Chama cha Wanasayansi wa Kilimo-Mazao Tanzania (CROSAT) umefunguliwa Disemba 4 jijini Arusha na Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Peter Pinda, ambapo amesema ni wakati wa watafiti kuhakikisha kuwa matokeo ya tafiti hayabaki kwenye maktaba bali yanawafikia wakulima moja kwa moja ili kuongeza tija na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
![]() |
| Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Peter Pinda akizungumza katika ufunguzi huo |
Mhe Pinda amesema mafanikio ya Taifa katika kilimo yatatokana na ushirikiano wa karibu kati ya watafiti, wataalamu wa ugani na wakulima.
Amesema kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu, “Kuendeleza Uzalishaji wa Mazao Yanayostahimili Mabadiliko ya Tabianchi Kupitia Usimamizi Endelevu wa Udongo na Rasilimali za Maji,” inaendana kikamilifu na mkakati wa Taifa wa kujenga kilimo chenye tija, kisasa na chenye uwezo wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi.
![]() |
| Rais wa CROSAT akizungumza katika mkutano huo |
Kwa upande wake, Mtafiti mbobezi katika tafiti za Kilimo Hai kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof. Kalunde Sibuga, ambaye pia ni Rais wa CROSAT, amesema chama hicho kilisajiliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1992 lakini kilipitia changamoto za kiuchumi ambazo zilisababisha kusimama kwa shughuli zake.
Ameongeza kuwa mwaka 2022 chama kilifufuliwa upya, kikasasisha nyaraka zake na kufanya Mkutano Mkuu wa Kwanza ambao uliweka msingi wa kulijenga upya chama hicho cha kitaaluma.
![]() |
Prof. Sibuga amesema tangu kufufuliwa kwake, CROSAT kimepitisha Katiba mpya mwaka 2023 na kuandaa Mpango Mkakati mwaka 2024 unaoongoza dira na mwelekeo wa chama. Amesema hadi mwaka 2025 chama kina wanachama 294, wakiwemo watafiti, wahadhiri, taasisi za utafiti, vyuo vikuu ikiwemo SUA, Serikali za Mitaa na sekta binafsi.
Amesema dhamira ya CROSAT ni kufanya kazi kwa karibu na Wizara ya Kilimo, taasisi za utafiti kama TARI, vyuo vya kilimo na wadau wa sekta binafsi ili kuhakikisha teknolojia, ubunifu na matokeo ya tafiti yanamfikia mkulima kwa wakati. Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kupanua matumizi ya teknolojia na kuongeza uzalishaji katika mnyororo wa mazao nchini.
Katika hatua nyingine, Prof. Sibuga amemuomba Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda kukubali kuwa Mlezi wa chama hicho kama ilivyoainishwa kwenye Katiba ya chama.







0 Comments