Na: Siwema Malibiche
Wanafunzi wanaosoma Chuo Kikuu
cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wametakiwa kuzingatia mafunzo kwa vitendo
yanayotolewa na Chuo hicho kwa kuwa
mafunzo hayo yatawasaidia kukuza ufanisi wa kiutendaji na kuendana na soko la
ajira lililopo nchini.
Hayo yamesemwa na Afisa Kilimo Idara ya Mimea Vipando na Bustani SUA Bw. Wensislaus Milinga wakati akizungumza na SUAMEDIA kwenye Kampasi ya Edward Moringe Sokoine Mkoani Morogoro alipokuwa akisimamia mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Shahada ya Awali ya Uzalishaji na Usimamizi wa Mazao wakati wa mafunzo ya kuandaa shamba la mbogamboga.
Bw. Milinga amesema mafunzo kwa
vitendo yanayotolewa chuoni hapo yana malengo mazuri na makubwa katika
kuzalisha wataalamu wenye ujuzi katika sekta ya kilimo.
Aidha, ameongeza kuwa SUA
imeleta mafunzo kwa vitendo mapema kwa wanafunzi wapya wa mwaka wa kwanza ili kujua uwezo na uelewa wao juu ya kilimo huku akibainisha
kuwa kuna mwitikio mkubwa kwa wanafunzi hao kushiriki katika mafunzo ambapo
inawasaidia kutunza kumbukumbu kwa kuhusianisha kile wanachokifanya shambani na
watakachokisoma darasani.
Kwa upande wake Mwanafunzi wa
Mwaka wa Kwanza wa Shahada ya Uzalishaji na Usimamizi wa Mazao Bw. Nais Isaya
amekipongeza Chuo Kikuu cha SUA kwa kuandaa mazingira mazuri ya kuwawezesha
wanafunzi kufanya mafunzo kwa vitendo ikiwemo mashamba ya kujifundishia wanafunzi
yanayowasadia kuwajengea uwezo katika uzalishaji kwa kutumia teknolojia
mbalimbali kuanzia shambani hadi sokoni.
Nao wanafunzi wa Mwaka wa kwanza wa Shahada hiyo ya Uzalishaji na Usimamizi wa Mazao Bi. Elizabeth Salimu na Bi. Elvira Rwechungura wamewataka wanafunzi wote kushiriki ipasavyo katika mafunzo kwa vitendo huku wakieleza kuwa kilimo kinaweza kufanyika na mtu yeyote bila kujali jinsia
.Wameongeza kuwa wanawake wanatakiwa kujikita zaidi katika kuhudhuria na kushiriki katika mafunzo kwa vitendo na kutokata tamaa kwa kutambua kuwa fursa zinazopatikana kwenye kilimo zinaweza kumnufaisha mtu yeyote awe mwanamke au mwanaume.
0 Comments