Na:
Winfrida Nicolaus
Wataalamu
na taasisi zinazohusika na utoaji wa taaluma na utafiti wa miti wametakiwa
kuishawishi Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzisha stoo ya mbegu
ya miti ya asili ya muda mrefu ili kuepuka kuendelea kupoteza miti hiyo
kutokana na uharibifu mkubwa katika misitu ya asili.
Akijibu
hoja mbalimbali zilizotolewa kwenye mjadala katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya
kuanzishwa kwa Kitivo cha Mafunzo ya Misitu
katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Kamishna Msaidizi Mwandamizi
wa Uhifadhi na Meneja sehemu ya Biolojia ya Mbegu za Miti kutoka Wakala wa Huduma
za Misitu Tanzania (TFS) Fandey Mashimba amesema kwa sasa kasi ya uharibifu wa
misitu na miti ya asili ni kubwa hivyo ipo haja ya wadau kutoa ushawishi kwa
mamlaka ili kutengenezwa stoo itakayosaidia kutunza mbegu hizo.
“Ni
dhahiri kuwa kila kukicha misitu ya asili inazidi kuteketea kutokana na
shughuli za kibinadamu ambapo mti kama mvule, mninga pamoja na mpingo
inaendelea kupotea bila taifa kuhifadhi mbegu zake” amesema Mashimba.
Aidha
amesema ipo haja ya watoa maamuzi na watunga sheria kutumia wataalamu wa misitu
katika kutoa maamuzi na kutunga sheria zinazolenga kulinda na kuhifadhi misitu
ili weweze kuwashauri ipasavyo juu ya masuala yote yanayohusu sekta ya misitu.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mstaafu wa Misitu na Nyuki Dkt. Felician Kilahama akitoa
uzoefu wake kwenye sekta ya misitu amesema hakuna namna yoyote ya kufanya
endapo wataalamu hawatasikilizwa na kuthamini michango yao katika kudhibiti na
kukabiliana na uharibifu wa misiti unaosababisha mabadiliko ya tabianchi.
Dkt.
Kilahama amesisitiza kuwa misitu ya asili ni misitu wezeshi kwenye sekta nyingine
na kwamba baadhi ya mambo mengi yanayohusu misitu yanakwama kutokana na mifumo
iliyopo nchini hasa kwenye utashi wa kisiasa.
0 Comments