SUAMEDIA

Wasindikaji wa chakula nchini wametakiwa kutumia tafiti za SUA kukuza ubora wa bidhaa zao

 Na: Siwema  Malibiche

Wasindikaji wa chakula nchini wametakiwa kutumia tafiti, teknolojia na maabara  zilizopo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)  ili kukuza ubora wa bidhaa wanazozalisha  na kuleta matokeo mazuri kwa mlaji na kupanua soko lao kibiashara.



Hayo  yamebainishwa na Mratibu wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam SUA  Dkt. Doreen Ndosi wakati wa warsha ya siku mbili inayofanyika katika Kampasi ya Edward Moringe Sokoine Mkoani Morogoro inayohusisha wataalamu kutoka SUA, wajasiriamali  na wabunifu kutoka kongano mbalimbali mkoani humo.

Dkt. Ndosi amesema lengo kuu la warsha hiyo ni kupitia kwa kifupi andiko linaloonesha namna gani watafanya kazi katika Kituo cha Kiteknolojia cha kusindika chakula.

Aidha Dkt. Ndosi  amebainisha kuwa SUA imeanzisha Kituo cha Kiteknolojia cha kusindika chakula (Agrifood Technology Station) ambacho kitatumika kama kiwanda cha kuzalisha mazao ya chakula kwa kusindika chakula kutoka kwa wasindikaji mbalimbali ambapo kitahusika na  usindikaji wa chakula kwa mazao ya mimea na nafaka kwa kutengeneza unga na bidhaa nyingine.

Amesema SUA inatarajia kufanya kazi na watu wengi kwa namna tofauti kwa kushirikiana na kwa kutumia kituo hicho cha kiteknolojia ambapo wajasiriamali wote wanakaribishwa kutumia wataalamu, tafiti na mashine  zinazopatikana chuoni hapo ili kuleta faida kwa mjasiriamali mmoja mmoja  na SUA kama Taasisi.



Kwa upande wake Afisa Mratibu wa Tafiti kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH) Bi. Minza Charles amesema wao kama tume wamekuwa na ushirikiano mzuri na SUA katika kuleta andiko lililowakusanya wajasiriamali na wabunifu pamoja huku akisema kama taasisi  inawakaribisha wajasiriamali kutumia Kituo cha Kiteknolojia cha Kusindika Chakula kutoka SUA ili kuboresha uzalishaji wa chakula  kwa kutumia huduma zake ikiwemo huduma za kisayansi na kiteknolojia .

Naye Mkurugenzi Mtendaji kutoka kongano la uzalishaji wa nafaka mkoani Morogoro  Bw. Alexander Jekoniah, ameupongeza uongozi wa Chuo kwa warsha hiyo na kutoa fursa kwa wajasiriamali kutumia maabara zilizopo chuoni hapo katika uzalishaji wa bidhaa na anaamini kupitia  Kituo cha Kiteknolojia cha kusindika chakula kutoka SUA itasaidia kutumika kwa virutubisho asilia katika kuandaa unga badala ya kutumia virutubisho kutoka nje ya nchi.

Kwa upande wake mjasiliamali kutokea Morogoro  Bi. Esther Muffui  ameishukuru SUA  kwa kuanzia warsha  hiyo na kukiri kuwa kwa sasa watu wengi wanatamani kula vyakula vinavyokidhi ubora na amewataka wajasiriamali wote kutembelea  SUA katika Idara ya Sayansi ya Chakula ili kupata ushauri wa kitaalamu utakao wawezesha kuzalisha bidhaa zenye ubora stahiki kwa mteja ili kukuza afya.







Post a Comment

0 Comments