Na: Farida Mkongwe
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Samia Suluhu Hassan amezindua kitabu cha Hayati Edward Moringe Sokoine
kiitwacho “Edward Moringe Sokoine: Maisha na Uongozi Wake” na kuwataka viongozi
wote wakiwemo vijana kukisoma kitabu hicho ili wapate mafunzo ya uaminifu, nidhamu
na uchapakazi ambayo ni alama iliyoachwa na Hayati Sokoine.
Rais Samia ametoa kauli hiyo
Septemba 30, 2024 wakati akizindua kitabu hicho katika Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam na kusema Hayati Sokoine
alikuwa ni Kiongozi mwenye nidhamu, mzalendo, mwaminifu, muadilifu, mchapakazi,
aliyedumisha mila na mpenda haki hivyo watanzania hawana budi kusoma kitabu
hicho ili waweze kuiga misingi ya uongozi kutoka kwa Hayati Sokoine.
Rais Samia amesema kwa mujibu
ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 asilimia 81.21 ya watanzania wapo
chini ya umri wa miaka 40 kwa maana kwamba kati ya kila watanzania 5 waliopo sasa ni mmoja tu ndiyo alikuwa hai
wakati Sokoine anafariki dunia mwaka 1984, hivyo ni muhimu kutunza na kusimulia
vizuri kumbukumbu za shujaa huyo ili vijana waweze kusoma na kujifunza uongozi kupitia historia yake.
“Kitabu hiki tunachokizindua
leo sio tu kinaonesha maisha ya kiongozi huyu mashuhuri bali pia fikra, mawazo
yake, kazi zake, changamoto alizokutana nazo, na jinsi alivyojenga misingi
imara ambayo nchi yetu inaendelea kunufaika nayo hadi sasa”, amesema Mhe.
Samia.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amewasihi watanzania na wadau wote wa maendeleo kusoma kitabu cha Hayati Sokoine ili wapate mafundisho na kuyatumia katika kuboresha utendaji wao wa kazi na kuleta maendeleo yatakayoimarisha Taifa na kuleta ustawi wa wananchi.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu
cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda amesema ili kuendelea
kumuenzi na kukumbuka fikra za Hayati Sokoine, tangu mwaka 1992 Chuo hicho
kimekuwa kikiandaa kila mwaka Mhadhara wa Kumbukizi ya Sokoine ambapo April 8,
2024 Chuo kilifanya Mhadhara wa Kumbukizi ya miaka 40 ya kifo cha Sokoine ambao
ulienda sambamba na hafla ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwa SUA.
Kitabu cha “Edward Moringe Sokoine: Maisha na
Uongozi Wake“ kilichoandaliwa kwa ushirikiano wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo (SUA) na Taasisi ya UONGOZI ambacho
kinaangazia safari ya Kiongozi huyo
kuanzia Makuzi yake katika jamii ya Kimasai hadi nyadhifa za Uongozi wake ikiwemo
Waziri Mkuu kina Sura 14, Kurasa 499 na jumla ya watoa taarifa 57 walihojiwa
katika kufanikisha uandishi wa kitabu hicho.
0 Comments