Na: Tatyana Celestine
Uongozi
wa Kampuni ya Uzalishaji wa Sukari Bagamoyo ulio chini ya Makampuni ya Bakhresa
umekipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwa kutoa wahitimu ambao
wanaaminika kwa kiwango kikubwa katika mnyororo mzima wa uzalishaji wa bidhaa
ya Sukari.
Akizungumza
na Kitengo cha Mawasiliano na Masoko SUA, Meneja Rasilimali Watu wa Kiwanda cha
Sukari Bagamoyo Bw. Habibu Issah amesema kuwa kiwanda chao chenye malengo ya
kuzalisha tani Laki Moja kwa mwaka kimeridhishwa sana na ushirikiano kati yao
na SUA kwani umekuwa na tija kwa kuwaletea wanafunzi wanaojifunza kwa vitendo
ambao wanaongeza uzalishaji.
Bw.
Issah amesema ukiufuatilia mnyororo mzima wa uzalishaji wa Sukuri kuanzia
shambani, umwagiliaji, uwekaji wa mbolea, uvunaji na uchakatajiwa Sukari
yenyewe, kumekuwa na wahitimu na wanafunzi wanaofanya mazoezi kwa vitendo na wamekuwa
wakifanya kazi vizuri na sio mzigo katika utendaji wa kazi wao.
Aidha Meneja Rasilimali Watu huyo amesema kiwanda hicho ni cha kisasa na hata Teknolojia zake ni za kisasa lakini hakuna changamoto wanayopata wanapowapokea wanafunzi kutoka SUA kwani wanawapa mafunzo kidogo kama utaratibu wao na ni kwa sababu SUA imekuwa ikiwapatia nafasi ya kujifunza kwa vitendo mara kwa mara mafunzo ambayo yanawawezesha kujua teknolojia zinazoenda na wakati.
Kwa
upande wake Bw. Saguti Ibrahimu ambaye ni Mtafiti Idara ya Kilimo katika Kiwanda cha Sukari Bagamoyo na pia ni mhitimu kutoa SUA amesema chuo hichi ni
chuo bora kwa utoaji wa elimu kwani mafunzo waliyopata chuoni yametosha
kuwafanya watimize majukumu yao pamoja na kuwepo kwa teknolojia ngeni za kisasa
zaidi zinazoletwa na kiwanda.
Aidha amewaasa vijana kujiunga na chuo hicho na waondoe fikra kuwa kilimo ni cha jembe la mkono pekee kwani sasa kuna teknolojia za kisasa nyingi ambazo kijana anaweza kufanya kilimo katika maeneo mbalimbali kama wao walivyofanikiwa kufanya kazi katika viwanda hivyo wakione kilimo kama fursa tofauti na zamani.
Akizungumzia
lengo la kuwatembelea wanafunzi hasa katika Kiwanda cha Sukari cha Bagamoyo,
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko Bi. Suzana Magobeko amesema ni
kujionea namna wanafunzi wahitimu na wanaofanya mafunzo kwa vitendo ili
kuboresha mitaala yake zaidi.
Amesema pamoja
na kupokea pongezi kutoka kwa kiwandani lakini SUA inaona fahari kushikirikiana
na Sekta binafsi kama Makampuni ya Bakhresa ambayo yamekuwa na mchango mkubwa
katika uchumi wa nchi kwa kuzalisha bidhaa mbalimbali zinazotokana na mazao ya
kilimo lakini pia kwa kujenga muhusiano ikiwa ni pamoja na kubadilishana
uzoefu, SUA kuleta wanafunzi wajifunze kwa vitendo na kiwanda kinapokuwa na
nafasi za ajira basi wanafunzi wa SUA wapewe nafasi.
0 Comments