Na: Calvin Gwabara – Morogoro.
Mradi wa Utafiti wa kuongeza
matumizi ya taarifa za bioanuai kwa uhifadhi endelevu na kipato kwenye Milima
ya Tao la mashariki nchini Tanzania wabaini uwepo wa zaidi ya Bioanuai 3935
kwenye Misitu ya asili ya hifadhi ya Kilombero,Uzungwa na Uluguru.
Mkuu wa mradi huo wa utafiti Prof. Pantaleo Munishi kutoka Idara ya Mifumo Ikolojia na Uhifadhi katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo akitoa matokeo ya utafiti huo. |
Akitoa takwimu hizo wakati wa
ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa maafisa uhifadhi kutoka kwenye misitu hiyo
mitatu ya asili ya hifadhi iliyo kwenye Safu za milima ya Tao la mashariki, Mkuu
wa mradi huo wa utafiti Prof. Pantaleo Munishi kutoka Idara ya Mifumo Ikolojia
na Uhifadhi katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo amesema matokeo hayo ya
utafiti yatasaidia wahifadhi kutambua na kuweka mikakati ya namna ya kutunza
bioanuai hizo na kuzitangaza ulimwenguni ili kuongeza tija.
“Milima ya Tao la mashariki ni
moja ya maeneo muhimu ya Bioanuai yanayotambulika
kidunia na kupewa kipaumbele ili kutunzwa na kumekuwapo kwa miradi mingi ya
utunzaji wa misitu na Bioanuai zilizomo lakini kumekuwa hakuna taarifa sahihi
za Bioanuai zilizomo katika kipindi chote cha utekelezaji wa miradi hiyo”
alifafanua Prof. Munishi.
Aidha amesema kuwa taarifa
zilizopo pia hazipo sehemu moja kiasi cha kuwa rahisi wahitaji kuzipata
kirahisi hivyo kuchangia kupunguza jitihada za kuzitangaza lakini pia
kuzihifadhi hasa katika kipindi hiki mabacho mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa
makubwa na kupelekea kuathiri bioanuai nyingi na zingie kupotea.
Mtafiti huyo mkuu amesema baada
ya kukamilisha utafiti wao wa kuzitambua bioanui zinazopatikana kwenye misitu
hiyo mitatu ya hifadhi ya asili iliyo kwenye milima ya tao la mashariki
wameamua kuwaita maafisa uhifadhi kutoka misitu hiyo na kuwapatia lakini pia
kuwafundisha namna bora za kutumia mifumo ya kimtandao kuzitangaza ili
zifahamike duniani kote na kutunzwa.
Akifungua mafunzo hayo ya siku
tatu Mkurugenzi mstaafu wa Idara ya
Misitu na nyuki wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Ezekiel Mwakalukwa amesema
kuwa matokeo mazuri ya utafiti yakitunzwa vizuri katika sehemu moja na
kuwezesha kupatikana kirahisi yanaweza kusaidia jamii na Serikali kufanya
maamuzi sahihi ambayo yataleta tija kwa Wananchi na Taifa.
Mkurugenzi mstaafu wa Idara ya Misitu na nyuki wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Ezekiel Mwakalukwa ambaye ni mhadhiri mwandamizi kutoka SUA akifungua mafunzo hayo. |
“Bioanuai ni rasilimali muhimu sana kwa
maendeleo ya jamii na taifa na mara nyingi kutokuwa na taarifa zake sahihi katika
nchi au misitu kunapelekea uhifadhi wake kuwa mgumu na zingine kutoweka hivyo
tafiti zinasaidia sana kuzitambua lakini kuweka mipango madhubuti ya
kuzihifadhi ili ziendelee kutoa mchango stahiki kwenye maendeleo” alieleza Dkt.
Mwakalukwa.
Aliongeza “Nipongeze kazi kubwa
iliyofanywa na Mradi huu unaaongozwa na Prof. Pantaleo Munishi kutoka hapa SUA
kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kufanya utafiti katika misitu yetu mitatu ya
hifadhi ya asili iliyo kwenye milima ya Tao la mashariki kubainisha bioanuai
muhimu zilimo na kuwezesha taarifa zake kupatikana na hivyo kuwa rahisi
kuzitangaza dunaini na kusaidia mipango ya serikali na wasimamizi wa misitu
hiyo kupanga mipango bora ya kuzihifadhi”.
Nae bwana Alan Kimbita ambaye ni
afisa mipango na mawasiliano kutoka Mfuko wa Uhifadhi wa Milima ya Tao la
Mashariki (EAMCEF) ambao ndio wafadhili wa mradi huo wa utafiti wamepongeza
kazi nzuri iliyofanywa na watafiti hao kutoka SUA na Chuo Kikuu Huria cha
Tanzania kwa kuja na taarifa hizo muhimu na hivyo kuwezesha kutambua Bioanuai
zilizopo kwenye maeneo hayo kwa sasa.
Alan Kimbita ambaye ni afisa mipango na mawasiliano kutoka Mfuko wa Uhifadhi wa Milima ya Tao la Mashariki (EAMCEF) akitoa neno la shukrani kwa watafiti hao. |
“Baada tu ya kuchapisha baadhi ya
viumbe hai waliobainika kwenye misitu hiyo tayari tumeanza kupata maswali
kutoka maeneo mbalimbali duniani wakitaka kujua vinapopatikana na hii ni ishara
njema kuwa kama taarifa zote zitakusanywa hivi na kutangazwa kikamilifu
zitavutia wadau wengi sana kuja kuzitembelea kuziona na wengine kufanya tafiti
na kusaidia uhifadhi” alisema Kimbita.
Utafiti huo umebainisha bioanuai
za Mimea,Ndege,Wnyama,Mijusi na vingine na kupitia mafunzo hayo wataweza kuweka
mikakti ya kuhakikisha vinatangazwa kwenye mitandao yote na kuwekwa kwenye
mfumo wa taarifa za bioanuai za Tanzania (TanBIF) na ule wa dunia yaani (BGIF).
Picha ya pamoja na Mgeni rasmi na washiriki wa mafunzo hayo ambao ni maafisa wa uhifadhi kutoka misitu mitatu ya hifadhi ya asili iliyofanyiwa utafiti na Mradi huo. |
0 Comments