Na: AYOUB MWIGUNE
Wanafunzi wa kidato
cha tatu wanaosoma somo la kilimo kutoka Shule ya Sekondari Wilbalda iliyopo
Kabuku mkoani Tanga wametembelea Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na kupata fursa ya kuona namna kilimo kinavyofanyika kwa vitendo kupitia somo la kilimo ambalo linafundishwa shuleni kwao pamoja na kukuza ufahamu wao juu ya shughuli zinazofanywa na Chuo hicho .
Hayo yameelezwa
na Venance Peter ambaye
ni Mwalimu kutoka shule hiyo wakati
akizungumza na SUAMEDIA kuhusiana na lengo la kutembelea SUA kwa wanafunzi
wanaosoma somo hilo.
Mwl. Peter amesema
kimsingi shule yao inafundisha somo la kilimo hivyo wameona ni vyema kwa
wanafunzi hao kuweza kutembelea Chuo Kikuu cha SUA kwa ajili ya kuweza
kujifunza kwa vitendo kwa wanafunzi hao kwani SUA ina vifaa vya kisasa
ambavyo kwa taasisi nyingine hawana,
mfano mashine ya kukamua maziwa ya ng’ombe pamoja na kuwa na wataalam waliobobea katika kilimo.
“Tumeweza kujifunza ufugaji wa Sungura,
Nguruwe, Kuku pamoja na Ng’ombe kuanzia kuzaliwa kwake mpaka ukuaji wake, vile
vile tumepata nafasi ya kujifunza uzalishaji wa samaki, samaki anapotaga mayai
mpaka hatua ya mwisho.” amesema mwl. Peter.
Aidha Mwl. Peter
amesema SUA imewapa wanafunzi wao mwangaza na kurejea shuleni kwao Wilbalda
tayari wakiwa wamejaa ujuzi na maarifa kuhusu somo la kilimo na anaamini
wanafunzi hao wataenda kuwa mabalozi wazuri kuhusiana na Chuo hicho.
Vile vile Mwl. Peter ametoa
wito kwa shule nyingine nchini ambazo zinafundisha somo la kilimo kuweza
kukitumia Chuo Kikuu cha SUA katika
kukuza uelewa kwa walimu wa masomo hayo pamoja na wanafunzi katika kujifunza
kwa vitendo ambapo wao wameweza
kunufaika kwa kwa kiasi kikubwa hali itakayowasaidia katika kukuza shughuli zao
za kilimo.
Kwa upande wake Epiphania
Sembeka ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu kutoka shule hiyo amesema wamejifunza mambo mbalimbali katika
ufugaji sambamba na namna ya kuweza kuikinga mifugo na magonjwa mbalimbali
hivyo kupitia SUA amepata mwangaza wa
kile wanachojifunza darasani ambapo wameongeza maarifa ya kutosha hivyo ametoa
rai kwa wanafunzi wenzake kutunza maarifa waliyoweza kuyapokea chuoni hapo .
“Nawashukuru SUA kwa
elimu ambayo wametupatia itaweza kutusaidia kwa baadaye tuweze kuwa watu
wakubwa katika kilimo ambapo tutajenga uchumi wa taifa.” amesema Seberua
Maganga mwanafunzi wa shule hiyo.
0 Comments