Na: Farida Mkongwe
Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo
Kayanza Pinda amewataka viongozi wa
Kanda ya Mashariki na wananchi kwa ujumla kuvitumia vizuri Vyuo Vikuu kikiwemo
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Vyuo vya Kati na Vyuo vingine vya
ngazi ya chini vilivyopo mkoani humo katika kuendeleza Sekta ya kilimo nchini.
Mhe. Pinda ametoa kauli hiyo Agosti 8, 2024 wakati akifunga Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere mjini Morogoro na kusema kuwa Kanda hiyo ina bahati kubwa ya kuwa na vyuo vikuu vingi na kwamba kinachotakiwa ni kujipanga ili kuweza kuzitumia rasilimali zilizopo katika vyuo hivyo.
“Bahati nzuri Kanda hii mna
bahati kubwa sana, mna vyuo vikuu, vyuo vya kati na vyuo vingine vya ngazi ya
chini, kubwa zaidi ndani yake ni uwepo wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo,
hawa ndiyo wanaibua vichwa vinavyokuja baadaye kusimamia shughuli za kilimo,
uvuvi na ufugaji, kwenu ni tuzo kubwa, kinachotakiwa ni kutafuta namna ya
kuzitumia tuzo hizo ili zitupeleke mbele ”, amesema Mhe. Pinda
Kabla ya kufunga Maonesho hayo
Mhe, Pinda alitembelea mabanda mbalimbali likiwemo banda la SUA na kujionea
shughuli mbalimbali zinazofanywa na banda hilo ikiwa ni pamoja na tafiti na
teknolojia ambazo zinaongeza tija katika uzalishaji wa mifugo na mazao ya
kilimo.
Katika Maonesho ya Nanenane ya
mwaka huu Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeibuka mshindi wa pili kwa
upande wa Taasisi za Mafunzo na Utafiti, mshindi wa kwanza ni Taasisi ya
Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) na mshindi wa tatu ni Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA).
Akizungumzia ushindi huo
Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza (ICE) SUA Dkt. Devota Mosha amewashukuru
washiriki wote wa Maonesho ya Nanenane kwa banda la SUA na kusema kuwa
wanajipanga ili mwakani wawe washindi wa kwanza kama ilivyo kawaida yao.
“Nichukue nafasi hii kuwashukuru
washiriki wote kwa sababu tumekuwa na mambo mengi mapya na watu wamefurahia
sana labda changamoto kubwa ambayo tumeiona ni wenzetu TARI kuwa na vipando
vingi zaidi yetu, niwaombe washiriki wote wa SUA tuimarishe vipando vyetu ili
mwakani tuendelee kushinda nafasi ya kwanza kama ilivyokuwa kwa miaka ya nyuma”,
amesema Dkt. Devota.
0 Comments