SUAMEDIA

Wanachama na Wadau wa Chama cha Taaluma ya Sayansi ya Kilimo Mazao Tanzania (CROSAT) wafanya Mkutano wao wa pili jijini Dodoma

Na: Tatyana Celestine Manda

Wanachama na Wadau wa Chama cha Taaluma ya Sayansi ya Kilimo Mazao Tanzania (CROSAT) Desemba 19, 2023 wameanza Mkutano wao wa pili jijini Dodoma katika kuhakikisha maendeleo ya Kilimo na Teknolojia za Kilimo nchini zinawasaidia wakulima, watumiaji wa mbegu na viuatilifu ili kuwepo na matumizi sahihi na salama ya viuatilifu pamoja na upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima.


Rais wa Chama cha Taaluma ya Sayansi ya Kilimo Mazao Tanzania (CROSAT)  Prof. Kallunde Sibuga akizungumza wakati wa mkutano ulioanza rasmi 19.12.2023 jijini Dodoma.


Akizungumza na waandishi wa Habari Rais wa Chama hicho Prof. Kallunde Sibuga amesema kuwa mkutano huo umelenga kuwaleta karibu watafiti, wakulima, vikundi vya wakulima, wagani , wanafunzi pamoja na wote wanaojishughulisha na sayansi ya mimea kwa lengo ya kuipitia katiba ya chama hicho na kuafikiwa iweze kusajiliwa na vyombo vya Serikali.


Aidha amesema kuwa lengo lingine ni kutengeneza mpango mkakati ambao utasaidia kuendeleza chama hicho na kuhakikisha sayansi mimea inakuwa sehemu muhimu katika kuendeleza shughuli za kilimo nchini ili kuleta tija kwa watumiaji wa Sayansi ya Kilimo na Mazao Tanzania.


Prof. Sibuga amesema kuwa kupitia mkutano huo wadau  watashiriki semina maalumu ambayo itatolewa na wabobezi katika masuala ya mbegu, matumizi bora ya viuatilifu kwa lengo la kutoa ufafanuzi katika maeneo hayo muhimu kama lengo la wanasayansi wa mimea na mazao kuangalia sera ya nchi inavyosema na wao kujikita katika kutatua changamoto zinazojitokeza.


Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI  ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wataalamu wa Sayansi ya Mazao Tanzania Patrick Ngwediagi alipotakiwa kujibu swali linalolenga changamoto ya upatikanaji wa mbegu kulingana na teknolojia kwa sasa amesema kuwa makampuni yanajitahidi kutengeneza mbegu lakini wakulima wanasita kutumia mbegu bora kwa sababu mbegu hizo ni ghari.


Aidha Katibu Mkuu huyo amewasihi wakulima wasisite kujiunga na Chama cha CROSAT kinachoweza kuwasadia kufahamu mambo mbalimbali ambayo ni faida kwao ikiwemo matumizi ya mbegu bora kwa matokeo chanya bila kujali bei ya mbegu iliyoko sokoni kwani mbegu hizo zitawaletea faida kubwa kwenye kilimo  tofauti na matumizi ya mbegu zilizo zoeleka na kukosa tija katika kilimo.


Nae Mkulima Mzalishaji Mbegu za Maharagwe Lishe kutoka Kagera Wilaya ya Misenyi Bw.  Deusdedit Stephen amesema kuwa kuna umuhimu wa kujiunga na Chama cha CROSAT kwani ni kitovu cha wataalam wa mazao pia ni sehemu pekee wataalam wanapokutana kuunganisha mnyororo wa uzalishaji unaosaidia kuwaweka kwenye masoko na kwamba kwake imempa faida na njia ya kufikisha mahitaji kwa wakulima na walaji.


Aidha ameongeza kuwa kujiunga na chama hicho kunaongeza tija ya kutatua changamoto mbalimbali shambani hivyo chama kinatoa nafasi ya kuunganisha mawazo kwa pamoja kushambulia changamoto kama wadudu, uharibifu wa mazao, na kuyakabili magonjwa kabla hayajasambaa.


Nae Prof. Eliningaya Kweka kutoka Taasisi ya Mimea na Viwatilifu amesema kuwa Mamlaka ya Mimea (TPHPA) wameona kuna umuhimu wa kushirikiana na CROSAT kwani watapata taarifa sahihi kwa wakati stahiki pamoja na kupata taarifa za pembejeo bila kusahau taarifa za matumizi ya pembejeo (viuatilifu) ambazo hazikusajiliwa na kusaidia kuzuia kuendelea kutumika kwa usalama wa mazao na afya ya binadamu.


Mkutano huo utafuatiwa na Semina Maalumu itakayofanyika Desemba 20, 2023 itakayoangazia matumizi sahihi na salama ya viuatilifu, upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima ambapo Mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe.









Post a Comment

0 Comments