SUAMEDIA

Mradi wa Utafiti wa "FETE" kuja na majibu ya Mazingira ya Chakula na Lishe kwa nchi zinazoendelea.

 Na: Calvin Gwabara – Morogoro.

Jopo la Watafiti katika Mradi wa Utafiti wa Mazingira ya Chakula katika Miji na kuboresha lishe ya Walaji (FETE) wamekutana kuzindua mradi na kupanga mikakati ambayo itasaidia kuimarisha lishe ya jamii na kupunguza utapiamlo kwa nchi nne za Afrika zinazoshiriki utafiti huo.

Mtafiti Mkuu wa mradi wa utafiti wa (FETE) kwa upande wa Tanzania Prof. Joyce Kinabo akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo.

Hayo yamebainishwa na Mtafiti Mkuu wa mradi huo kwa upande wa Tanzania Prof. Joyce Kinabo ambaye ni Profesa wa lishe wakati akitoa utambulisho wa Mradi huo kwa jopo hilo linalohusisha watafiti kutoka Tanzania, Ghana, Afrika ya Kusini,Malaysia na Ujerumani kwa ufadhili wa Shirikisho la Shirika la Kilimo na Chakula la Ujerumani (BLE).

“Wengi mtakubaliana na mimi kuwa tuna matatizo makubwa ya utapiamlo wa chini na utapiamlo wa juu kwa maana kwamba uzito ulikithiri na unene unazidi kuwa changamoto kwa watu wengi hapa Tanzania changamoto ambayo inachangiwa na mazingira hafifu na mabaya ya chakula”, alieleza Prof. Kinabo.

 “Vyakula vingi ambavyo tunaviona kwenye maduka yetu na supermarket vingi ni vile vya kusindikwa na vingi vinakuwa na sukari nyingi,Mafuta mengi na hivyo kusababisha mlaji kuchukua wanga au sukari zaidi ya mahitaji ya mwili wake na hii humfanya  mtu aongezeke uzito kwa kasi na hivyo kupelekea kupata magonjwa yasiyo ya kuambukizwa mfano Kisukari, Shinikizo la damu na magonjwa ya moyo”, aliongeza Prof. Kinabo.

Hivyo amesema utafiti huo unalenga kuboresha mazingira ya masoko na maeneo yote yanayouza chakula ili waweze kuuza vyakula ambavyo vitampatia mlaji lishe bora kama vile matunda, mbogamboga na jamii ya mikunde na sio vyakula ambavyo vinaenda kumuongezea matatizo  hasa vilivyosindikwa sana na kuongezea sukari nyingi na mafuta mengi.

Prof. Kinabo amesema kuwa utafiti huo utatoa somo na suluhisho la nini kifanyike kwa upande wa wadau, Sera, na wauzaji wa vyakula ili kwa pamoja waweze kuipa jamii chakula kitakachosaidia kuimarisha lishe za afya za watu.

Amesema Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kinanufaika hasa kupitia wafanyakazi wake kupata ufadhili wa masomo katika shahada za Uzamivu lakini pia wanataaluma watafiti kwenye mradi huo kupata nafasi ya kuchangamana na wenzao kutoka nchi zingine na kuongeza uzoefu na mashirikiano katika maeneo ya utafiti.

Akizungumzia kilichowasukuma kutekeleza mradi huo wa utafiti Mratibu wa Mradi huo kwa nchi zote nne Dkt. Daniella Waible kutoka Taasisi ya Uchambuzi wa Masoko ya Thenen ya nchini Ujerumani amesema ni tatizo kubwa la utapiamlo,Ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza na hasa zinazoathiri ukuaji wa uchumi ambapo tabia za kilishe zinapitia mabadiliko makubwa.

Mratibu wa Mradi huo kwa nchi zote nne Dkt. Daniella Waible kutoka Taasisi ya Uchambuzi wa Masoko ya Thenen ya nchini Ujerumani akitoa neno wakati wa uzinduzi wa mradi.

“Lengo kubwa ni kuanzisha ushirikishaji wa tatizo na fursa, kuleta suluhisho la kutengeneza mazingira bora ya chakula, kutoa mfano wa marejeo, kutoa modeli ya marejeleo ya jinsi mbinu zilizoanzishwa na matokeo yaliyopatikana yanavyoweza kutumika kwa upana zaidi katika Kusini mwa dunia kwa kuwalenga watu wa hali ya chini mijini”, alifafanua Dkt. Daniella.

Mratibu huyo wa mradi huo wa utafiti amesema andiko la mradi kwa wafadhili liliwasilishwa toka mwaka 2019 na kupitia michakato mbalimbali na hatimae mwezi wa 12 mwaka 2022 ndio likakubaliwa na hivyo akatumia nafasi hiyo kuwashukuru wadau wote walioshiriki kwa uvumilivu na michango yao ya mawazo katika kufanikisha mradi huo muhimu kwa maendeleo ya nchi zote.

Akifungua mkutano huo Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Shahada za Juu, Utafiti na Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu (DRPTC) Prof. Esron Karimuribo kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda amepongeza uchaguzi wa mada ya Utafiti huo na kwamba umekuja wakati muafaka ambapo kumekuwa na changamoto kubwa ya ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukizwa yanayohusishwa na lishe duni.

Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Shahada za Juu, Utafiti na Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu (DRPTC) Prof. Esron Karimuribo akifungua Mkutano wa uzinduzi wa mradi huo wa FETE.

“Tunashuhudia vifo vya watu wetu vinavyotokana na wao kutokujua mambo ya msingi tu ambayo yanahusiana na lishe hivyo sisi kama nchi lakini pia katika ukanda huu tunapongeza mada ya utafiti huu mliyochangua kwakuwa inakwenda kujibu changamoto hizo ambazo zinaathiri afya za jamii zetu”, alifafanua Prof. Karimuribo.

Hata hivyo kwa niaba ya Uongozi wa SUA, Prof. Karimuribo amewahakikishia watafiti hao ushirikiano wa kutosha katika kufanikisha utekelezaji wa mradi na kuwaeleza kuwa wamechagua mahali sahihi kutokana na Chuo hicho kuongoza kwa miaka mitano mfululizo kwenye masuala ya Utafiti na machapisho nchini Tanzania hivyo wanafanya kazi na taasisi bora nchini.

Jopo la watafiti wa Mradi huo wa FETE linajumuisha watafiti na wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo nchini Tanzania,Taasisi ya uchambuzi wa Masoko ya Thunen ya Ujerumani, Taasisi ya Utafiti wa masuala ya Sera za  Sayansi na Tenolojia (STEPRI) ya nchini Ghana, Chuo Kikuu cha Nottingham cha Malaysia na Chuo Kikuu cha KwaZulu – Natal cha Afrika ya Kusini.

Picha ya pamoja ya jopo la watafiti kutoka nchi tano zinazotekeelza mradi huo wa utafiti 

Mtafiti Mkuu wa Mradi huo kwa upande wa Tanzania Prof. Joyce Kinabo (Kushoto) akipokea zawadi kutoka Ujerumani kwa niaba ya wanajopo hilo zilizokabidhiwa na  Dkt. Johanna Schott.






















Post a Comment

0 Comments