SUAMEDIA

Utafiti wa Mradi wa EFLOWS waonesha maji yanapungua kwenye mito

 Na: Calvin Gwabara – Mbarali.

Matokeo ya Utafiti wa miaka miwili kuangalia Mtiririko wa maji na afya ya Mto Mbarali Mkoani Mbeya yameonesha kuwa Maji yanapungua na hii ni kutokana na ongezeko la watu na mahitaji ya matumizi ya maji kuongezeka sambamba na uharibifu wa vyanzo vya maji vya mto huo.

Mtafiti Mkuu wa Mradi wa EFLOWS Prof. Japhet Kashaigili akiwasiliasha matokeo ya utafiti huo mbele ya wadau kwenye warsha iliyofanyika Wilayani Mbarali Mkoani Mbeya.

Hayo yamebainishwa na Prof. Japhet Kashaigili kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ambaye ni Mtafiti Mkuu wa Mradi huo wa miaka miwili wa Utafiti  wa Usimamizi Endelevu wa Madakio ya Maji Kupitia Tathmini ya Kuimarisha Mtiririko wa Maji kwa Mazingira na Utekelezaji wake katika Kulinda Ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi na Athari za Shughuli za Kibinadamu Tanzania (EFLOWS) wakati akiwasilisha matokeo ya utafiti huo kwa wadau wa maji wa mto Mbarali wilayani humo Mkoani Mbeya.

“Tulichokiona kwenye utafiti ni kwamba wingi wa maji kwenye mto unaendelea kupungua, wahitaji wa maji wanaongezeka lakini pia mabadiliko ya tabia nchi nayo yameathiri kwa kiasi kikubwa mtawanyiko wa maji na mvua kwenye maeneo haya na hivyo kupelekea maji kupungua mtoni na athari zake hasi zikionekana kwenye mifumo ikolojia ya mto hasa wakati wa kiangazi. Tumeona uwepo wa matumizi makubwa ya maji bila vibali kwa kutumia pampu, na uzalishaji mkubwa wa mchanga wakati wa mvua kutokana na shughuli za kibinadamu kwenye maeneo ya vyanzo milimani na kwenye mashamba” alisema Prof. Kashaigili.

Aliongeza” Shughuli za kibinadamu zinazofanyika Mbarali kwa maana ya makazi, kilimo, ufugaji, ufyatuaji wa matofali kwenye vyanzo vya maji na mtoni, kilimo cha vinyungu, moto na shughuli zingine za kibinadamu zimechangia kwa kiasi kikubwa mtawanyiko wa maji kwenye mto, lakini uchukuaji wa maji kwenye mto ndio umeonekana kuongoza kwa athari hasi”.

Prof. Kashaigili amesema changamoto hiyo ya matumizi makubwa ya maji imepelekea mto kukauka kabisa maeneo ya chini wakati maeneo ya juu ya mto na katikati ukifika unakuta maji mengi yanatiririka ambayo hayafiki mwisho yanaishia njiani kutokana na watu kuyachepusha na kuyachota kwaajili ya shughuli zao mbalimbali hususani kilimo ambacho hakizingatii matumizi sahihi ya maji hayo.

“Kwa maana hii ni kwamba Mto Mbarali hauchangii chochote kwenye Mto Ruaha Mkuu hasa wakati wa kiangazi kwenye maeneo ya uhifadhi na hii maana yake ikolojia ya mto na uendelevu wake imeathirika na hivyo kushindwa kufikia malengo makubwa ya Kidunia ya maendeleo endelevu na yale ya kitaifa ya kuifadhi na kuilinda baonuai ya mto” alifafanua Mtafiti huyo Mkuu Prof. Kashaigili.

Mtafiti huyo aliyebobea kwenye tafiti za Masuala ya maji na Mazingira Duniani amesema pamoja na Utafiti kutoa matokeo hayo kwa wadau hao muhimu pia wameainisha njia na mikakati ya kufanya ambayo ikifanyika itasaidia kupunguza athari zilizojitokeza na kusaidia kurejesha afya ya mto na mtiririko wa maji kwenye Mto Mbarali na mingine nchini kwa kuwa changamoto zinafanana.

Amesema moja kati ya mikakati hiyo ilikuwa kurejesha uoto wa asili kwenye vyanzo vyote vya maji vilivyoathirika na kingo za mito, ambapo mradi kwa kuanzia umesaidia kuanzisha vitalu vikubwa viwili vya miti rafiki wa maji kwenye wilaya ya Wanging’ombe Mkoani Njombe na Mbarali Mkoani Mbeya kwa kutumia elimu asili na kufanikiwa kupanda miti zaidi ya elfu 45 kwenye vyanzo na kingo za mito pamoja na kuanzisha ufugaji wa nyuki kwa ajili ya kuongezea kipato cha jumuiya za watumia maji wanaosimamia madakio pamoja na kuongezea uhifadhi.

Kwa upande wake Mtaalamu wa Sayansi za maji na Viumbe wake kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Bw. Sherald Mkama ambaye alikuwa anaangalia afya ya mto na usalama wa maji kupitia mradi huo amesema matokeo yameonesha maji yanayotiririka kwenye mto huo bado ni salama kwa kuwa baada ya kufanya utafiti wamekuta viumbe ambao hawawezi kuishi kwenye maji ambayo sio salama.

Mtaalamu wa Sayansi za maji na Viumbe wake kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Bw. Sherald Mkama akizungumzia matokeo hayo mbee ya Waandishi wa habari nje ya mkutano huo.

“Viumbe wadogo wanaoishi majini pamoja na samaki wanauwezo mkubwa wa kutoa ishara ya ubora wa maji katika eneo na ndio maana pamoja na watafiti wengine huchukua sampuli za maji na kuzipima, lakini mbinu ya kuangalia viumbe ndio muhimu zaidi kwa kuwa ndio wanakaa kwa muda mrefu kwenye eneo hilo kuliko kupima maji maana unaweza kwenda kuchota maji ukakuta wakati huo ni bora kwa muda huo tu, ila viumbe waishio kwenye maji hawapiti wapo muda wote” alifafanua Mkama.

Mtafiti huyo amezitaka mamlaka zinazosimamia maji kuhakikisha kunakuwepo na usimamizi mzuri hasa kwenye maeneo wanayochota maji mengi kwenye skimu ya Umwagiliaji ya Igomelo ambayo wanatumia viuatilifu na mwisho sehemu ya maji hayo yanarudi mtoni yakiwa na viambata sumu kama hawatazingatia matumizi salama ya viuatilifu, mwisho yaweza pelekea kuua viumbe walio mtoni na kuathiri pia jamii inayotegemea maji ya mto huo kwa matumizi ya nyumbani.

Naye Mtafiti aliyekuwa anaangalia mimea iotayo kandokando ya mito na vyanzo vya maji Dkt. Emmanuel Mwainunu kutoka Taasisi ya utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) amesema mimea hiyo ni muhimu kwa kuwa ndiyo inayosaidia kuwepo kwa uhai wa mto kwa kutunza maji, kufyonza mbolea na kuyafanya yatiririke kidogokidogo badala ya kasi pamoja na kuzuia mmomonyoko wa kingo za mito.

Mtafiti aliyekuwa anaangalia mimea iotayo kandokando ya mito na vyanzo vya maji Dkt. Emmanuel Mwainunu kutoka Taasisi ya utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) akizungumzia eneo la utafiti wake.

“Tunapoangalia hali ya Uoto kwenye mito na afya ya mto huwa tunatumia madaraja A mpaka F, hivyo tunaposema hali ya ukanda fulani ni A maana yake hakuna uharibufu katika eneo hilo, lakini ikiwa daraja B ina maana eneo limeanza kupata athari za awali lakini hazijaanza kuleta madhara, na ikishuka kufikia daraja D ina maana athari ni kubwa sana na ikifikia daraja F ina maana eneo hilo limeharibika sana, athari ni kubwa sana na madhara yake ni makubwa sana ambapo si rahisi kurekebishika katika hali ya kawaida. Tathmini yetu imeonesha kuwa yapo mabadiliko kadhaa ambayo yametokana na shughuli za kilimo na ufugaji lakini kimsingi uharibifu wake kwenye uoto wa kandokando za mto sio mkubwa sana na kupelekea kupata daraja B,  hata hivyo ni lazima jitihada zifanyike kusitisha changamoto hii kuendelea” alieleza Dkt. Immanuel.

Amesema kuwa wamekuta mimea kama vile Msandali ambayo ni mimea yenye matumizi mengi kama utengenezaji wa Manukato pamoja na mimea mingine rafiki wa maji lakini inawezekana kutoweka kwa kuwa jamii zinafanya shughuli mbalimbali kandokando ya mto huo na kuiathiri, hivyo jitihada za makusudi zichukuliwe na mamlaka za usimamizi wa mito kunusuru mto kuachwa wazi.

Mradi huu wa Utafiti unatekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na kutekelezwa katika Bonde la mto Rufiji ndani ya dakio la mto Mbarali kwa ushirikiano na Bodi ya Maji ya mto Rufiji, jumuiya za watumia maji, Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Wilaya ya Mbarali na Wanging`ombe na jamii, kwa ufadhili wa program ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa, UNEP, kupitia michango ya nchi kumi wanachama wa Azimio la Nairobi ambapo kwa Tanzania ni kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, katika kutekeleza Mpango Mkakati wa Kivitendo wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi chini ya uratibu wa Sekretarieti ya Azimio la Nairobi.



Post a Comment

0 Comments