SUAMEDIA

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ruvu watembelea SUA, wasifu mafunzo kwa vitendo yanayotolewa Chuoni hapo

Na: Farida Mkongwe

Wanafunzi 60 wa Shule ya Sekondari Ruvu iliyopo mkoa wa Pwani wametembelea banda la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwenye Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayofanyika mjini Morogoro na kukisifu Chuo hicho kwa namna kinavyotoa mafunzo kwa vitendo sambamba na kutumia Teknolojia za kisasa ambazo zinawasaidia wakulima.



Wakizungumza na SUAMEDIA Agosti 7, 2023 mara baada ya kutembelea banda hilo wanafunzi hao akiwemo Helena Domonick Oswald na Delfine Deusdedith Pius wanaosoma kidato cha sita mchepuo wa CBA wamesema wamejifunza mambo mbalimbali kuhusu Kilimo,U na Uvuvi na kwamba sasa wameamini kuwa SUA ni Chuo bora cha Kilimo hapa nchini.

“Wito wangu kwa wanafunzi wengine kuhusiana na Chuo cha SUA, SUA ni chuo kizuri kina wataalamu waliobobea lakini pia Chuo kina Teknolojia nzuri za ufundishaji, kuna vitu vingi ambavyo vinapatikana SUA lakini sehemu nyingine havipatikani kwa mfano Panya buku wanaotambua makohozi ya kifua kikuu na mabomu ya ardhini, kwa kweli SUA ni Chuo bora hata ukiangalia majengo yake ni mazuri”, amesema Helena Oswald.

Kwa upande wake Mwanafunzi Delfine Pius amesema amevutiwa sana na mafunzo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi yanayotolewa na SUA kwa kuwa yanaonesha uhalisia wa nini Chuo hicho kinafanya kwa wakulima na kwamba amefurahishwa zaidi kuona vifaranga vya samaki kwani alikuwa akivisikia tu na sasa ataenda kuwaeleza wanafunzi wenzake kuhusu ufugaji wa Samaki aina ya Sato.

“Mimi nawaambia wanafunzi wenzangu wasome kwa bidii wafaulu vizuri ili wajiunge na SUA kwani Chuo hiki kina ufaulu mzuri na kinamjenga mwananfunzi aweze kupata ajira iwe kujiajiri mwenyewe au kuajiriwa”, amesema Delfine

Naye Mwalimu Amon Mahona anayefundisha Somo la Kilimo katika Shule hiyo ya Sekondari ya Ruvu ambaye ameambatana na wanafunzi hao amesema wameamua kutembelea banda la SUA kwa sababu  SUA ni Chuo cha Kilimo ambacho kina mambo mengi ya kujifunza.

“Sisi kule tunawafundisha wanafunzi kwa nadharia lakini hapa wenzetu wanajifunza kwa vitendo zaidi na kuna teknolojia za kisasa kwa kweli wanafunzi wamefaidika kwani kubwa zaidi wamejua namna ya kuchagua kozi zao baada ya kumaliza kidato cha sita”, amesema Mwalimu huyo.






Post a Comment

0 Comments