SUAMEDIA

Wakulima washauriwa kutumia Teknolojia za kisasa katika uvunaji misitu

Na: Farida Mkongwe

Wakulima wameshauriwa kutumia Teknolojia za kisasa na za kitaalamu kuweza kupasua miti au kuburuza magogo badala ya kukata miti mingine kwa ajili ya kupasua mti mmoja ili miti inayobakia iendelee kukua kwa faida ya baadae.


Bw. Ramadhani Sudi, Fundi Mchundo kutoka Idara ya Uhandisi Misitu na Sayansi ya Wanyama iliyopo Ndaki ya Misitu, Wanyapori na Utalii katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) akionesha Teknolojia ya kisasa ya uvunaji misitu inavyofanya kazi.

Ushauri huo umetolewa Agosti 7, 2023 na Bw. Ramadhani Sudi, Fundi Mchundo kutoka Idara ya Uhandisi Misitu na Sayansi ya Wanyama iliyopo Ndaki ya Misitu, Wanyapori na Utalii katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wakati akizungumza na SUAMEDIA katika Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi maarufu kama Nanenane Kanda ya Mashariki mjini Morogoro.

Bw. Sudi amesema kwa sasa kuna Teknolojia ya kisasa ya uvunaji misitu inayorahisha uvunaji mbao misituni kwa kutumia kifaa kinachojulikana kama sawmill structure ambacho humfanya mkuliama kupasua mti anaoutaka na kuiacha mingine ikiendelea kukua.

Kitendo hiki kinafanywa na watu wachache tofauti na siku za nyuma kwamba kitendo cha kuuangusha mti na kuuhamisha kuupeleka pale ambapo zitachanwa mbao kinafanywa na watu wengi sana lakini sasa teknolojia hii imekuja kumrahisishia mvunaji inaweza kufanywa akiwa mtu mmoja au wawili au watatu kulingana na ukubwa wa gogo lakini si zaidi ya watu hao.

Akielezea sababu ya kutengeneza teknolojia hiyo Bw. Sudi amesema kabla ya hapo watu wengi walikuwa wanavuna magogo lakini kabla ya kuvuna walikuwa wanalazimika kukata miti mingine midogo kutengeneza milunda (mishamu) kwa ajili ya kusukuma gogo kulipeleka sehemu ya upasuaji kwa kuiburuza kitendo ambacho kilikuwa kinaathiri miti midogo inayoendelea kukua pamoja na nyasi zilizopo eneo hilo.

Hii mashine anaweza kutengeneza mtu yeyote kwa sababu haina gharama kubwa na malighafi zinazotumika ni zile zinazotumika mtaani na lengo letu watu waone na ikiwezekana watengeneze ili kusudi tuweze kuilinda misitu yetu, amesema Bw. Sudi.

                           

                           

                            




Post a Comment

0 Comments