SUAMEDIA

Wakulima washauriwa kupima udongo ili kulima kwa tija

 

Na: Farida Mkongwe

Wakulima wameshauriwa kujenga mazoea ya kupima udongo kabla ya kulima ili kujua virutubisho vilivyopo kwenye udongo ambavyo vitawasaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu aina ya mazao yanayofaa kupandwa ambayo yataleta tija kwenye mavuno.

                        

Ushauri huo umetolewa Agosti 2, 2023 na Mkuu wa Maabara ya Sayansi za Udongo kutoka Idara ya Sayansi za Udongo na Jiolojia iliyopo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Amour Suleiman wakati akizungumzia huduma zinazotolewa na Idara hiyo katika Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki yanayofanyika katika viwanja vya Nanenane mjini Morogoro.

Bw. Suleiman amesema pamoja na kupima udongo pia mkulima anapaswa kujua aina ya virutubisho vilivyopo kwenye mbolea atakayoitumia pamoja na kiwango kinachohitajika kwenye udongo kwani sio kila mbolea inatumika kwenye kila udongo unaotumika kwa kilimo.

Tunawakaribisha kwenye banda letu hapa mtaweza kujionea teknolojia ambazo tupo nazo za kisasa zaidi tunazotumia katika upimaji wa sampuli zetu sambamba na hilo pia tunatoa huduma ya kupima bure udongo na maji na kutoa majibu hapa hapa kwenye banda letu lakini ni kwa baadhi tu ya vipimo si vipimo vyote ambavyo tunaweza kupima hapa, amesema Bw. Suleiman.

Aidha Mkuu huyo wa Maabara ya Sayansi za Udongo kutoka SUA amewataka wakulima wanaotumia maji ya kisima kumwagilia mashamba yao kuhakikisha maji hayo yanapimwa ili kuepukana na changamoto zinazoweza kujitokeza.

Kumwagilia maji ya kisima yasiyopimwa kunaweza kusababisha kuweka tatizo ambalo halikuwepo katika udongo wako, unaweza kukuta maji yana chumvi kali sana ukakuta unahamishia ile chumvi kwenye udongo na udongo wako usiweze kufaa tena kwa matumizi ya kilimo kwa sababu kuja kuurudisha kwenye hali yake ya kawaida itakugharimu kwa kiasi kikubwa mno, amesema Bw. Suleiman.

 


 





 

Post a Comment

0 Comments