SUAMEDIA

Wakulima waishio mijini watumie njia rahisi ya Kibanda Mazao kupanda Mazao

 Na Winfrida Nicolaus

Chuo Kikuu Cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Idara ya Mimea na Vipando imewarahisishia wakulima hasa wale waishio mijini kutumia njia rahisi ya Kibanda Mazao kupanda Mazao ya aina mbalimbali na kwa kiwango cha ubora katika sehemu moja ndani ya eneo dogo na kuweza kujikwamua Kiuchumi.





Amesema hayo Bw. Isack Kazosi Afisa Kilimo kutoka Idara ya Mimea na Vipando SUA wakati akizungumza na SUAMEDIA katika Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere mjini Morogoro kuhusiana na Teknolojia mbalimbali za uzalishaji wa vipando ikiwemo mazao ya muda mrefu na mazao ya muda mfupi.

 

Bw. Kazosi amesema wapo kwenye Maonesho hayo kwa lengo la kutoa Elimu kwa wananchi pamoja na kuonesha Teknolojia mbalimbali ikiwemo ya Kibanda Mazao ambayo ni njia rahisi hasa kwa watu waishio mijini  ambao hawana mashamba kuwahabarisha kuwa kuna uwezekano wa kupanda mboga mboga za aina tano katika Eneo dogo na kuweza kufanya biashara au kula wenyewe na familia zao.

“Tunaonesha na kutoa Elimu ya jinsi gani mkulima anaweza akazalisha kwa Tija na kuongeza kipato ili kuhakikisha kuwa mahitaji yake ya kila siku ya familia anaweza kuyamudu kupitia Kilimo katika Mazingira yoyote yale iwe mijini au vijijini, iwe unalo shamba au hauna cha muhimu ni kuwatumia Wataalam vizuri na kuzingatia njia za kitaalam”, amesema Isack Kazosi.

Kazosi ameongeza kuwa licha ya kufundisha mbinu na kanuni bora za Kilimo pia kuna Mfumo wa Umwagiliaji kwa njia ya matone ambayo jamii inaweza kwenda Banda la SUA kwenye maonesho hayo ya Nanenane Kanda ya Mashariki kujionea na kuelekezwa namna sahihi ya kutumia ili kukabiliana na changamoto ya aina yoyote ile kutokana na mabadiliko ya tabianchi.



Kwa upande wake Bw. Robert Kabati Muhitimu wa Chuo Kikuu Cha Sokoine cha Kilimo SUA ambaye kwa sasa ni Mhandisi wa Umwagiliaji na Rasilimali Maji na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya NEGLO inayojihusisha na kutengeneza na kuuza vifaa vya Kidijitali pamoja na kufunga Mifumo ya Kisasa kwenye Mashamba amewataka wananchi kutembelea Banda la SUA ili kujifunza Teknolojia walizonazo na namna gani wanavyoweza kushirikiana na SUA katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili Wakulima.


Amesema imekuwa ni hamasa yake kubwa kushirikiana na SUA tangu akiwa shuleni hivyo kupitia Bunifu anazozifanya ikiwemo ya Mfumo wa Umwagiliaji ambapo ukifika Banda la SUA katika Idara hiyo ya Mimea na Vipando utaikuta imekuwa na manufaa kwa Wakulima hivyo anawahamasisha wanafunzi waliomaliza Vyuo Vikuu hasa SUA kuwa wabunifu ili kuweza kujiajiri na kuajirika.

     


Post a Comment

0 Comments